Bodi ya Azam Football Club, imemtangaza, Octavi Anoro, (42), kama Mtendaji Mkuu (CEO) mpya wa klabu, kwa mkataba wa miaka miwili, hadi 2027.
Nafasi hiyo ilikuwa wazi kufuatia aliyekuwa akiishikilia, Abdulkarim Nurdin maarufu kama Popat, kupandishwa cheo na kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Anoro, raia wa Hispania, anakuja na maarifa na uzoefu mkubwa wa kimataifa katika nyanja ya maendeleo ya utawala na biashara ya mpira wa miguu.
Aidha, Bodi pia imemteua, Rashid Seif Mohamed, kuwa msaidizi wa Mtendaji Mkuu (Assistant CEO).
Rashid ni mhitimu wa Shahada ya Umahiri ya utawala wa michezo (Master’s in Sports Management) pamoja na ngazi ya pili ya ukocha kutoka chama cha soka cha England, FA.
Uteuzi huu ni muendelezo wa harakati za klabu kujipambanua kiweledi katika ukuaji wa kimkakati na kuweka alama muhimu kwenye mageuzi ya kiuongozi kwa ajili ya ustawi wa muda mrefu.



