MARSEILLE: NDOTO ya Newcastle United ya kushinda mechi nne mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya imevunjika usiku wa kuamkia leo baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Olympique de Marseille, shukrani kwa mabao mawili ya mkongwe Pierre-Emerick Aubameyang.
Harvey Barnes aliwapa Waingereza hao mwanzo mzuri katika uwanja wa Stade Vélodrome baada ya kufunga dakika ya tano, akifunga bao lake la nne katika mechi zake tatu zilizopita kwenye mashindano yote.
Hata hivyo, Aubameyang alipindua mchezo ndani ya dakika nne mwanzoni mwa kipindi cha pili, akiipa Marseille ushindi wao wa pili wa msimu huu kwenye Champions League.
“Hatukuanza vizuri. Tulipaswa kufanya bora zaidi katika dakika 10 za kwanza, Baadae tulianza kuudhibiti mchezo. Kocha alituambia tuendelee ‘kupush’, nafasi zingetokea. Na hilo lilithibitika mara tu kipindi cha pili kilipoanza.” – Aubameyang aliambia Canal+.

Baada ya ushindi wao wa mechi tatu mfululizo bila kuruhusu bao, Newcastle walikuwa wanatafuta rekodi ya ushindi wa nne mfululizo jambo ambalo halijawahi kutokea kwao kwenye Champions League.
Kikosi cha Eddie Howe kilipata bao la mapema pale Barnes alipotumia vyema krosi ya Sandro Tonali. Dakika mbili kabla ya bao hilo, beki Malick Thiaw alikuwa karibu kuifungia Newcastle, lakini kiungo wa Marseille Pierre-Emile Højbjerg aliokoa mpira juu ya mstari wa goli.
Licha ya makosa ya pasi mwanzoni, Marseille walianza kutawala mchezo hatua kwa hatua. Aubameyang alipoteza nafasi kadhaa katika kipindi cha kwanza, kabla ya kujisahihisha kipindi cha pili.

Mshambuliaji huyo wa Gabon alisawazisha dakika ya 46 baada ya kumzunguka kipa Nick Pope, aliyekuwa mbali na lango, kabla ya kupiga kombora kutoka pembeni na kutinga nyavuni.
Dakika nne baadaye, Aubameyang alimalizia kwa ustadi mpira uliopigwa na Timothy Weah kwenye mwamba wa karibu, na kuwaduwaza vijana wa Eddie Howe.
The post Newcastle yakwama Marseille first appeared on SpotiLEO.









