Aime Bigiraneza, mchezaji chipukizi wa klabu ya daraja la pili ya Burundi Les Gêpiers du Lac, alianguka uwanjani na afariki dunia juzi tarehe 20 Desemba 2025.
Kisa hicho kilitokea wakati wa mechi ya ligi dhidi ya Amasipiri Never Give Up FC kwenye Uwanja wa kituo cha Ufundi mjini Bujumbura.
Bigiraneza inasemekana alianguka uwanjani wakati wa mchezo huo na kukimbizwa hospitalini na baadaye kukutwa na umauti.
Wakati ripoti rasmi za matibabu zinasubiri, ripoti za mapema kutoka nchini humo zinaonyesha hali ya kutatanisha inayozunguka janga hilo kuwa huenda mchezaji huyo aliagizwa na makocha wake kucheza na sarafu mdomoni, jambo ambalo linashukiwa kuchangia kifo chake, pengine kwa kubanwa au kuzuiwa.
Tukio hilo limezua taharuki kubwa katika jamii ya soka ya Burundi, huku wadau mbalimbali wa michezo na vyombo mbalimbali wakieleza rambirambi zao.






