Ikiwa ni siku ya nne tangu michuano hii ianze, nimemsikia Rais wa Young Africans akitoa sifa lukuki kwa kile kilichofanyika na Taifa la Morocco, hususan katika ufunguzi wa mashindano na miundombinu iliyotumika.
Nami naongeza sifa hizo ziende pia kwa mataifa shiriki, kutokana na maandalizi mazuri na ushindani mkubwa unaoonyeshwa na kila taifa.
Kwa michezo ya jana ya makundi C na D, rekodi ya kipekee imewekwa baada ya idadi ya mabao kuongezeka, ambapo mabao 11 yalifungwa, huku michezo miwili pekee ikishuhudia clean sheet, ikipelekwa na Senegal na DRC.
Senegal wanaendelea kutoa somo la soka, huku DRC wakipata ushindi mwembamba uliotokana na ubora wa Benin. Sote tunakumbuka jinsi Benin ilivyoleta ushindani mkubwa kwenye kufuzu Kombe la Dunia; haikuwa rahisi kwa DRC kuondoka na ushindi huo.
Kwa upande wa Taifa Stars, ikiwa dhamira yetu ni kujenga timu shindani kuelekea AFCON 2027, kama alivyoeleza kocha Gamondi, basi kwa kile tulichokiona jana hatupaswi kurudi nyuma. Tumewafunga midomo wengi kwa kiwango cha mchezo tulichoonesha mbele ya Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe.
Hakika, mchezo wetu unaofuata dhidi ya Uganda utakuwa wa soka safi zaidi, pengine hata kuliko wa jana. Huu ndio mchezo mgumu zaidi kwetu, ukizingatia ushindani, uhasama na ukaribu wa kijirani kati ya mataifa haya mawili.
Tuendelee kujenga misingi hii, tusilale hata kidogo, kwani AFCON 2027 haiko mbali.
Imeandikwa na @mohusein_15
The post Kiwango Cha Taifa Stars Kinaridhisha, Wasirudi Nyuma appeared first on SOKA TANZANIA.





