DAR ES SALAAM: KLABU ya KMC FC imeendelea kufanya maboresho katika benchi la ufundi na idara ya uendeshaji baada ya kuwatambulisha rasmi Raphael Mpangala kuwa Kocha wa Makipa na Dalton Mgala kama Msimamizi wa vifaa wa timu hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuimarisha kikosi chake.
Kupitia taarifa iliyotolewa na klabu hiyo, uongozi wa KMC umeeleza kuwa ujio wa Mpangala unalenga kuongeza ushindani na ubora katika nafasi ya ulinzi wa mwisho, huku uzoefu wake katika kuwanoa makipa ukiaminiwa kuwa chachu ya kuboresha viwango vya wachezaji waliopo.
KMC imekuwa katika wakati mgumu kwenye ligi kwani ndio timu inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi yaani 14 katika michezo tisa ikishika mkia kwa pointi nne baada ya kushinda mchezo mmoja, sare moja na kupoteza michezo saba.
Kwa upande wa Dalton Mgala, klabu imesema uteuzi wake kama Msimamizi wa vifaa utasaidia kuboresha maandalizi ya timu, usimamizi wa vifaa pamoja na kuhakikisha mazingira bora ya kazi kwa wachezaji na benchi la ufundi kwa ujumla.
Uongozi wa KMC umeeleza kuwa mabadiliko hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa klabu kuimarisha mifumo yake ya ndani, kuongeza nidhamu ya kazi na kuweka mazingira yatakayowezesha timu kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya Ligi Kuu na michuano mingine itakayoshiriki.
The post KMC yatambulisha Kocha wa Makipa first appeared on SpotiLEO.




