PEMBA: GOLIKIPA wa Yanga SC, Abutwalibu Mshery, amewashukuru mashabiki wa klabu hiyo kwa sapoti kubwa waliyoipa timu yao, baada ya Yanga kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi jana, huku akisisitiza kuwa msimu bado ni mrefu na malengo makubwa bado yapo mbele.
Akizungumza mara baada ya kutwaa taji hilo, Mshery alisema mashindano ya mwaka huu yamekuwa ya kiwango cha juu na yenye ushindani mkubwa, jambo lililosaidia timu kujipima na kujiandaa vyema kwa msimu mzima.
“Kwa Wananchi, tumekuwa na mashindano bora sana ya Mapinduzi kama timu na kwangu binafsi. Nawashukuru sana kwa sapoti yenu kubwa kwetu kama timu na kwangu binafsi pia. Msimu bado ni mrefu, tuendelee kushikamana, Inshallah tutafikia malengo ya msimu,” alisema Mshery.

Katika michuano hiyo, Yanga haikupoteza mchezo hata mmoja tangu kuanza kwa Kombe la Mapinduzi, mafanikio ambayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uimara wa safu ya ulinzi pamoja na mchango wa magolikipa wake, akiwemo Mshery.
Licha ya kukaa benchi kwa muda mrefu kabla ya mashindano hayo, Mshery ameonesha wazi kuwa bado ni mmoja wa magolikipa bora nchini, akitumia fursa aliyopata kuonesha utulivu, uzoefu na uwezo mkubwa wa kulinda lango.
Ubingwa huo umeongeza morali kwa Yanga kuelekea mashindano yajayo ya ndani na kimataifa, huku Mshery akisisitiza mshikamano wa wachezaji na mashabiki kuwa ndiyo silaha kubwa ya kufanikisha malengo ya klabu msimu huu.
The post Mshery awashukuru mashabiki Yanga kwa sapoti first appeared on SpotiLEO.






