WINDHOEK:TIMU ya Taifa ya kriketi ya vijana chini ya umri wa miaka 19 (Tanzania U19) imeendelea kung’ara katika mechi za maandalizi ya Kombe la Dunia baada ya kuibuka na ushindi wa kusisimua wa wiketi moja dhidi ya Ireland U19 katika mechi ya pili ya maandalizi.
Katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa hadi mpira wa mwisho, Tanzania U19 ilionesha ujasiri, nidhamu na mapambano ya hali ya juu, hatimaye kuibuka na ushindi mwembamba lakini wa thamani kubwa dhidi ya wapinzani wao kutoka Ulaya.
Ushindi huo unaifanya Tanzania kumaliza mechi za mazoezi ikiwa na rekodi safi ya ushindi, baada ya awali kuifunga Japan U19 kwa mikimbio 81, hali inayotoa taswira chanya ya maandalizi na uwezo wa kikosi hicho kabla ya kuanza kwa mechi za makundi.
Kwa matokeo hayo, Tanzania U19 inaingia rasmi kwenye hatua ya makundi ikiwa na morali kubwa, kujiamini na matumaini mapya ya kuipeperusha vyema bendera ya Taifa katika jukwaa la kimataifa.
Michuano hiyo ya Dunia imeandaliwa na nchi za Zimbabwe na Namibia na tayari Tanzania wako Namibia. Wanatarajia kuanza michezo ya hatua ya makundi Januari 15 dhidi ya West Indies, baadaye Afrika Kusini na kuhitimisha kwa Afghanistan.
The post Kriketi Tanzania yaichapa Ireland U19 first appeared on SpotiLEO.





