DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Pedro Goncalves, amekoshwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake akisema wataendelea kupambana kushinda na kulinda heshima ya rangi zake.
Kauli yake hiyo inakuja baada ya Yanga kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa jana kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Amesema ushindi huo umetokana na dhamira ya pamoja ya kikosi kizima kuanzia benchi la ufundi hadi kwa wachezaji waliokuwa uwanjani, akisisitiza kuwa Yanga itaendelea kupambana kushinda na kulinda heshima ya rangi zake.
“Ni ushindi mkubwa uliopatikana kwa kujituma na kujitoa kwa hali ya juu kutoka kwa kila mmoja. Tunataka kuendelea kushinda na kuheshimu rangi za Yanga.”
Yanga ilitawala mchezo huo kwa kiwango kikubwa, ikionesha soka la kasi, pasi za uhakika na umakini mkubwa katika umaliziaji, hali iliyoifanya Mashujaa kushindwa kuhimili presha tangu dakika za mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
Ushindi huo uliipandisha Yanga kutoka nafasi ya pili hadi katika uongozi wa Ligi kwa kufikisha pointi 19.
Yanga kibarua kilichoko mbele yake ni Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Ijumaa watakuwa ugenini kuikabili Al Ahly ya Misri.
The post Kocha Yanga akoshwa kiwango cha wachezaji wake first appeared on SpotiLEO.




