KOCHA mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, ameonyesha utulivu na imani kubwa baada ya kumtaja winga mpya, Buba Jammeh, katika kikosi kilichosafiri kuelekea Rabat, Morocco, kwa ajili ya mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR Rabat.
Pedro amesema uamuzi wa kumjumuisha Jammeh umezingatia mahitaji ya timu katika mchezo huo mgumu, kuwa mchezaji huyo anaingia kikosini kwa mpango maalumu unaolenga kuongeza nguvu na ushindani katika safu ya ushambuliaji.
Kocha huyo raia wa Ureno amebainisha kuwa uzoefu, kasi na uwezo wa Jammeh kucheza katika nafasi tofauti za winga ni miongoni mwa vitu vilivyomvutia, akiamini vinaweza kuipa Yanga faida muhimu dhidi ya wapinzani wao wenye nguvu wakiwa nyumbani.
Pedro ameweka wazi kuwa hamuwekei presha kubwa mchezaji huyo mpya, akisisitiza kuwa anampa muda wa kuzoea mazingira ya timu, mfumo wa uchezaji pamoja na falsafa ya Yanga kabla ya kutegemea makubwa kutoka kwake.
Mbali na hilo, Pedro amegusia maandalizi ya jumla ya kikosi, amesisitiza kuwa Yanga imejipanga vyema kwa kuzingatia nidhamu, umoja na umakini mkubwa, mambo ambayo amesema yatakuwa silaha muhimu katika mchezo huo wa ushindani mkubwa.
Ameongeza kuwa wachezaji wake wanaelewa vyema ukubwa wa mechi dhidi ya AS FAR Rabat na wajibu waliobeba, huku kila mmoja akionesha ari ya kupambana ili kupata matokeo chanya yatakayoweka hai matumaini ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Kikosi cha Yanga kipo Rabat, Morocco, kikifanya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya wenyeji AS FAR Rabat, utakaochezwa Jumamosi ya Februari 7, ambapo macho na matarajio ya mashabiki wengi yameelekezwa kwenye kikosi hicho cha Jangwani.
The post PEDRO AWEKA DUA KWA BUBA MOROCCO appeared first on Soka La Bongo.




