Geita
Wananchi mkoani Geita wameshauriwa kuitumia Maabara ya Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kupima vifaa vya ujenzi vikiwemo Matofali na Kokoto.
Ushauri huo umetolewa na Fundi Sanifu wa Maabara wa TARURA mkoa wa Geita Bw. Robert Kunambi alipokuwa akitoa elimu kwa wananchi wanaofika kwenye banda la Taasisi hiyo lililopo kwenye Maonesho ya saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani hapa.
“Siku hizi kuna watengenezaji wengi wa Matofali, nawashauri wananchi kuleta sampuli ya matofali kutoka kwa watengenezaji tofauti tofauti ili tuyapime na kujiridhisha ubora wake kabla ya kuyatumia”.
Ameongeza kusema kwamba gharama za upimaji wa vifaa hivyo ni za chini ambazo kila mwananchi anaweza kuzimudu na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo ili kujenga nyumba zenye ubora zitakazo dumu Kwa muda mrefu.
Akiongea mara baada ya kupata elimu kuhusu maabara hiyo Mkazi wa Geita Bw. Mathia Chacha ameelezea furaha yake kwani awali alijua maabara hiyo ni kwaajili ya vifaa vya barabara tu.
“Sikuwa nafahamu kabisa kama vifaa vya ujenzi wa nyumba za makazi ya kawaida vinatakiwa vipimwe ili tujenge nyumba bora,nashukuru kwa elimu hii”.
TARURA inashiriki maonesho hayo ili kutoa elimu kuhusu majukumu yake pamoja na umuhimu wa kutunza miundombinu ya barabara ili iweze kutumika kwa muda mrefu.