Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), Janeth Mawinza, akionyesha vikoti wanavyovaa waendesha boda boda, Bajaji na madereva wa Daladala katika mradi wa Vunja Ukimya, Safari Salama bila Rushwa ya Ngono inawezekana uliozinduliwa leo Oktoba 10,2024 katika ofisi ya Kata ya Bunju jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), Janeth Mawinza, akionyesha stika wanazobandika waendesha boda boda, Bajaji na madereva wa Daladala katika mradi wa Vunja Ukimya, Safari Salama bila Rushwa ya Ngono inawezekana uliozinduliwa leo Oktoba 10,2024 katika ofisi ya Kata ya Bunju jijini Dar es Salaam.
KAMPENI ya Vunja Ukimya, Safari Salama bila Rushwa ya Ngono Inawezekana imezinduliwa leo, kwa lengo la kutokomeza rushwa ya kingono kwa wasichana pamoja na wanafunzi kwa ujumla.
Kampeni hiyo inasimamiwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Wanawake katika jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI) huku lengo ni kufikia wanafunzi 35,000 kutoka Shule sita za Kata ya Bunju, Dar es Salaam.
Mkurungezi wa taasisi hiyo, Janeth Mawinza, amesema kusudio la kampeni hiyo ni kutoa elimu kwa madereva wa daladala, bajaji na bodaboda, pia kutoa elimu ya ulinzi kwa wanafunzi shuleni kupinga rushwa ya ngono.
“Tunaamini kampeni hii italeta matokeo chanya katika vitu vitatu ambavyo tumelenga katika kutoa elimu kwa madereva ambao moja kwa moja ndio wanawabeba wanafunzi na wasichana kuwatoa sehemu moja kwenda nyingine, pia kuwapa ushawishi wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kutoa elimu ya ulinzi wa wasichana shuleni,” amesema Mawinza.
Akizungumza namna kampeni hiyo, ilivyoleta matokeo chanya katika Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni kuwa baada ya kupatiwa elimu hiyo, wameona mwitikio na mabadiliko makubwa dhidi ya ukatili wa kingono kwa wanafunzi.
Amesema kuwa wanahitaji kuwafikia wanafunzi wasiopungua 35, 000 katika shule sita ndani ya Kata ya Bunju A, kati yake Shule za Msingi nne na Sekondari mbili pamoja na kutoa elimu kwa madereva bodaboda wasio pungua 200 na walimu wasiopungua 100.
“Lengo ni ili kuhakisha wanakuwa salama pindi wanapokuwa kwenye vyombo vya usafiri.
Naye Ofisa wa Tadhimini na Ufuatiliaji kutoka katika taasisi hiyo, Hancy Obote, amesema maofisa ustawi wa jamii watasaidia kufahamu watoto wanaokutana na changamoto ya ukatili wa kingono katika kata hiyo, kwamba kazi yao inaendana na kampeni hiyo.
Ameeleza kuwa wamehusisha maofisa hao, ili kufanya kazi moja kwa moja na serikali kuhakikisha kuwa kampeni hiyo itaendelea hata baada ya taasisi ya WAJIKI kumaliza muda wao katika kata hiyo.
“Maafisa ustawi wa jamii na maofisa maendeleo ndio serikali yenyewe, hivyo tunaamini kuwa kampeni hii itakuwa endelevu hata ikatokea muda wetu umekwisha basi watakuwa tayari kuendelea na kampeni hii ya vunja ukimya, safari salama bila rushwa ya ngono ili kutokomeza ukatili huu,” amesema Obote
Ofisa ustawi wa jamii Kata ya Bunju, Lilian Chillo, amempongeza Mkurugenzi wa WAJIKI, kwa kuanzisha kampeni hiyo kwamba wameipokea kwa mtazamo chanya wakiamini itaenda kuleta mabadiliko katika Kata ya Bunju A, kama ilivyowanufaisha wengine.
Pia amesema wapo tayari kushirikiana na WAJIKI kuhamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi serikalini, hivyo wanaamini kuwa kampeni hiyo itawawezesha wanawake wa Kata ya Bunju kujitokeza.
“Nimefurahi kusikia kwamba kampeni hii sio kwamba imekuja kuanzia hapa Bunju A, imeshawafikia na kuwasaidia wasichana, wanafunzi wengi katika Mkoa wetu, mlianza kwenye Kata nyinginezo ambazo nimezisikia hapa na kuwa mmeona kuwa ni kwa namna gani watoto wetu wapo hatarini, hivyo tunapaswa kuwasaidia kwa njia hii, “amesema
Ofisa Ustawi wa Jamii Kata ya Bunju, Lilian Chillo akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Vunja Ukimya, Safari Salama bila Rushwa ya Ngono inawezekana uliozinduliwa leo Oktoba 10,2024 katika ofisi ya Kata ya Bunju jijini Dar es Salaam
Afisa Maendeleo Msaidizi Kata ya Bunju Jumanne Dindili, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa Vunja Ukimya, Safari Salama bila Rushwa ya Ngono inawezekana uliozinduliwa leo Oktoba 10,2024 katika ofisi ya Kata ya Bunju jijini Dar es Salaam.
Ofisa wa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Wajiki Hancy Obote, akizungumza wakati wa hafla hiyo.