KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda amezindua ofisi ya walipakodi binafsi wenye hadhi ya juu na kuwahakikishia huduma bora.
Mwenda alisema hayo Dar es Salaam, jana alipozindua ofisi hiyo iliyopo katika jengo la Golden Jubilee, Posta na kubainisha uzinduzi huo ni matokeo ya muundo mpya ulioidhinishwa na Serikali ya Awamu ya Sita,
“Ninayo furaha kuungana na nyie kuja kuizindua ofisi ya walipakodi binafsi wenye hadhi ya juu iliyoanza kazi Oktoba Mosi, mwaka huu,” alisema.
Alieleza ofisi hiyo itatoa huduma kwa walipakodi wa makundi manne ambayo ni wamiliki wa kampuni ambazo mauzo yake yanazidi sh. bilioni 20 kwa mwaka.
Walipakodi wengine watakaohudumiwa katika ofisi hiyo ni wamiliki wa hisa wanaomiliki hisa zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 2.5 kwa mwaka; wale wenye ubia wa kampuni ambao kama wana kampuni zinazidi sh. bilioni 20 kwa mwaka na viongozi wa miimili mitatu ya juu na wa taasisi watakaoteuliwa.
Kamishna Mkuu huyo alibainisha ofisi hiyo inawalenga walipakodi hao kwa sababu wanataka kuwapatia h2uduma bora.
Akifafanua kuhusu walipakodi wenye hadhi ya juu, alisema wamiliki wameanzisha kampuni ambazo zinalipa kodi katika mamlaka hiyo, wanalipa kodi kupitia mapato yao binafsi na ameajiri watu wanalipa kodi.
“Kwa kuanza tumeanza na walipakodi 158, lakini walipakodi wamiliki binafsi wapo 111 wote wameshaitwa, viongozi wa mihimili mitatu ya juu na wa taasisi watakuja baadaye 47,” alisema.
Aliongeza kuwa : “Tunawapa huduma bora kwani mchango wao mkubwa sana, wameanzisha kampuni, wanalipa kodi na viongozi wana mchango mkubwa wana majukumu mengi, lazima tuwarahishishie.”
Mwenda alisema lazima wawe karibu na walipakodi hao, kuhakikisha kile kinachotakiwa kulipwa kinalipwa.
Aliahidi huduma zitakuwa bora zinazoendana na hadhi yao na kuwaondolea usumbufu kwa kuwasogezea huduma karibu.
Naibu Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Mcha Hassan Mcha alisema ofisi hiyo ni miongoni mwa fursa ya kusogeza huduma karibu na walipakodi, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Pia, kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari walipakodi wajisikie kuwarahisishia kupata huduma na wawe tayari kulipa kodi kwa hiari hiyo ndiyo sababu ya kuanzisha ofisi hiyo.