Akizungumza katika Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yenye kaulimbiu “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi,” yanayofanyika katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe jijini Mbeya, Thwaiba Juma, Afisa kutoka Bodi ya Bima ya Amana (DIB), amesema kuwa wamekutana na machifu wa Mbeya pamoja na SACCOS ya waalimu jijini Mbeya na kubadilishana mawazo kuhusu jinsi wanavyoweza kusaidia wananchi kupata ufahamu kuhusu huduma zinazotolewa na Bodi ya Bima ya Amana.
“Tulitumia fursa hii kuwaelezea machifu majukumu yetu na umuhimu wa bodi katika jamii. Machifu walikubaliana kuwa ni muhimu elimu kama hii ifikie wananchi ili waweze kuelewa nafasi ya sekta ya fedha na umuhimu wa Bodi ya Bima ya Amana katika maisha yao,” amesema.
Aidha, aliongeza kuwa wanatambua kuwa wananchi wengi wanazo fedha ambazo wanaweza kuhifadhi benki, lakini wengi wao hawajui kwamba kuna usalama wa fedha zao kupitia Bima ya Amana endapo benki itakumbwa na changamoto.
Vilevile, alisema wa SACCOS ya walimu iliyopo jijini Mbeya, tumewapa elimu na kubadilishana nao mawazo na kuwaelezea majukumu na umuhimu wa Bodi ya Bima ya Amana.
“Pia walifurahia elimu hii na kutambua umuhimu wa kuhifadhi fedha zao benki, kwani fedha zinapokuwa benki zinapata ulinzi kupitia Bima ya Amana,” aliongeza.