Mahakama ya Israel ilisema Jumapili kwamba msemaji wa zamani wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amekamatwa kwa tuhuma za kuvujisha nyaraka za siri kwa vyombo vya habari bila kibali, jambo ambalo lingeweza kuathiri makubaliano ya kuwaachilia mateka waliokuwa wameshikiliwa huko Gaza.
Shirika la kijasusi la ndani la Shin Bet na jeshi lilianzisha uchunguzi kuhusu uvujaji huo Septemba mwaka jana, baada ya gazeti la Jewish Chronicle mjini London na gazeti la Ujerumani la Bild kuchapisha ripoti kulingana na nyaraka za siri za kijeshi.
Mamlaka ya Utangazaji ya Israel iliripoti kwamba baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Rishon LeZion kuamua kuondoa marufuku ya uchapishaji, iliruhusiwa kufichua kukamatwa kwa watu 4 katika kesi ya uvujaji wa nyaraka za usalama.
Mahakama ya Hakimu Mkazi ilisema kwamba Eli Feldstein alikamatwa pamoja na watu wengine watatu, wakiwemo maafisa wa usalama.
Kesi hiyo iliufanya upinzani kuhoji iwapo Netanyahu alihusika katika uvujaji huo, jambo ambalo Ofisi ya Waziri Mkuu ilikanusha.
Netanyahu alikanusha shutuma zinazohusisha wafanyakazi wa ofisi yake na alisema katika taarifa yake Jumamosi kwamba alifahamu kuhusu nyaraka hizo zilizovuja kupitia vyombo vya habari.
Moja ya ripoti hizo ilidai kufichua waraka unaoonesha kwamba kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar, ambaye baadaye aliuawa na Israel na mateka huko Gaza watatoroshwa nje ya Ukanda huo hadi Misri kupitia Ukanda wa Philadelphi kwenye mpaka wa Gaza na Misri.
Ripoti ya pili ilitokana na kile kilichosemekana kuwa mawasiliano ya ndani kutoka kwenye uongozi wa Hamas kuhusu mkakati wa Sinwar wa kuzuia mazungumzo ya kuachiliwa kwa mateka.
The post Msaidizi wa Netanyahu akamatwa baada ya uchunguzi,avujisha siri first appeared on Millard Ayo.