KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw.Gerson Msigwa,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati akizungumza nao leo Septemba 10,2024 jijini Dodoma kuhusu Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw.Gerson Msigwa,akizungumza leo Septemba 10,2024 jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusu Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la Kitaifa la Utamaduni linalotajia kuanza Septemba 20, na kumalizika Septemba 23,mwaka huu Mkoani Ruvuma ili kuimarisha Utamaduni uliopo nchini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw.Gerson Msigwa,wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 10,2024 jijini Dodoma kuhusu Tamasha la Tatu la Utamaduni la Kitaifa litakalofanyika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Bw.Msigwa amesema kuwa Kaulimbiu ya tamasha hilo itakuwa ni ‘Utamaduni wetu ni utu wetu, tuuenzi na kuuendeleza, Kazi iendelee’ Tamasha linaratibiwa na Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo waratibu wa Tamasha la Majimaji Serebuka, kutoka mkoani, Ruvuma Songea.
“Tamasha hilo litafunguliwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro,Septemba 20,mwaka huu na kilele chake itakuwa Septemba 23,mwaka huu na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan”amesema Bw.Msigwa