WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe (mb) amepiga marufuku wafanyabiashara wanaonunua kahawa kwa njia ya Kangomba na kuagiza wakamatwe huku akisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa katika zao hilo umelenga kuteka soko la kahawa ya Tanzania kimataifa.
Amesisitiza kuwa serikali kwa sasa inawekeza katika kahawa kwa kugawa miche na mbolea ya ruzuku hivyo,anatarajia kupigwa vita na wafanyabiashara kutokana na kukemea kangomba lakini hatarudi nyuma kwa maslahi ya zao hilo.
Waziri Bashe amesema hayo katika muendelezo wa ziara yake Mkoani Ruvuma mara baada ya kutembelea mashamba, viwanda vya kuchakata kahawa na skimu za umwagiliaji wilayani Mbinga na Nyasa.
βNajua haya maamuzi yatakuwa na maumivu na yatakuwa na kelele, mimi kelele nimezoea, kamateni wanaonunu kahawa kwa kangomba,βamesema.
Amesema, anatarajia vita kubwa dhidi ya wafanyabiashara wanaonunua kahawa kwa njia ya Kangomba na hatarudi nyuma.
βTutegemee kelele nyingi kutoka kwa wafanyabiashara lakini sipo tayari kuona kangomba katika kahawa.Kelele zitakuwa nyingi watapitishia kwa wakulima tujiandae lakini nasema ili kufikia soko la kimataifa hatuwezi kuvumilia ununuzi usiofaa,βamesema.
Amesisitiza kuwa, hatua ya serikali kuwekeza katika zao hilo, imelenga kuijengea ubora kahawa ya Tanzania kimataifa na kunufaisha wakulima.
βTunatoa mbolea na miche kwa ruzuku na kuwezesha kilimo hiki kuhimili ushindani dhidi ya kahawa za nchi nyingine,βamesema.
Akiwa katika miradi ya umwagiliaji inayotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Waziri Bashe amesemaβNimejionea kiwango cha umasikini wa watu wetu hapo mambo tumeanza kuyafanyia kazi.Tunamshukuru sana Rais Dk. Samia Suluhu Hasan kwa kutupatia fedha mwaka huu, nimemwambia Mbunge Injinia Stella Manyanya, tutafanyia kazi changamoto za watu wetu.
βTumeshatangaza na tumeshapata mkandarasi kwa skimu zenye hekta 8395 tutajenga barabara za ndani ya shamba, madaraja na vigawa maji ndani ya shamba na usanifu umeshakamilika na mkandarasi amepatikanaβ,amesema Waziri Bashe
Pia Waziri Bashe ameitaka,kufanya usanifu na kuziingiza barabara za Lipingo katika mpango wa utekeleza wa mradi huo wa Umwagiliaji
βNimegiza Tume ifanye usanifu, waingize kwenye mradi barabara zote mbili hapa Tume inatekelez miradi ya zaidi ya Bilioni 25 kwa Wilaya ya Nyasa pekee haishindwi kujenga hizo barabara zote,βamesema.
Aidha amesisitiza haja ya Skimu zilizopo katika Halmashauri ya Nyasa na idadi ya skimu zitakazo anza kufanyiwa utekelezaji kwa haraka.
βHalmashauri ya nyasa kuna skimu nane na kwa kuanzia tutaanza kuzijenga skimu mbili kuanzia mwaka huu wa fedha na ndani ya miaka 2 zote hizo zitakuwa zimejengwa.Muwape ushirikiano wataalamu wanaotekeleza miradiβ
βPia Tume mfanye ujenzi wa ghala katika eneo la mradi na mashine ya kukoboa mpunga ili wananchi waweze kuuza mchele badala ya Mpunga,βamesema.
Ameongeza kuwa Wizara ina mpango wa kuanza kuzalisha wa mbegu karibu na eneo la mradi wa Lundo katika kata ya Lipingo na kuanzisha vituo vya zana za kilimo na kujenga kituo cha mbolea.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Nyasa Injinia Manyanya, amesema Wilaya hiyo inahitaji kukua kiuchumi na tegemeo kubwa ni kilimo cha mpunga hivyo wanatarajia miradi ya umwagiliaji iwe chachu ya uzalishaji.