Kiasi cha shilingi 292,301,993.85 kinatarajiwa kutumika kwaajili ya kuanza ujenzi wa barabara ya kutoka Buzuruga kuelekea miti mirefu kwa urefu wa kilomita 0.4 kwa awamu ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa fedha za jimbo
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi mkandarasi eneo la kazi, zoezi lililofanyika katika barabara ya Buzuruga Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni matokeo ya maombi yake kwa serikali ya Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan na kufanikiwa kupewa fedha kwaajili ya ujenzi huo huku akiwataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji kuwa barabara hiyo itajengwa kwa fedha za wafadhili na si serikali
‘.. Nilipeleka maombi kwa barabara zaidi ya nne katika jimbo letu, Na bado tukaomba kilomita 12 kwa mheshimiwa Rais ambazo ziko nje ya hii, Pesa hii imetoka serikali kuu na sio mtu yeyote au mfadhili ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula amemtaka mkandarasi aliyepata kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kuhakikisha anaikamilisha kwa wakati, anazingatia ubora unaotakiwa pamoja na kuwatumia wananchi wa kata hiyo kwa kazi ndogo ndogo zisizohitaji utaalamu mkubwa ili nao waweze kunufaika na uwepo wa mradi huo
Kwa upande wake meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe J. Makonyo amefafanua kuwa mradi huo unatekelezwa na mkandarasi M/S JASSIE & COMPANYLIMITED ya jijini Mwanza kwa muda wa miezi sita kuanzia Agosti 26 hadi Februari 22, 2025 ambapo manufaa ya mradi huo yatakuwa ni kuongeza ubora wa huduma za usafiri kwa wananchi, kuvutia biashara, uwekezaji na kuongeza kasi ya ukuaji wa jiji la Mwanza
Mhandisi Musa Hamada ni mwakilishi wa mkandarasi anaetekeleza mradi huo kampuni ya M/S JASSIE & COMPANYLIMITED ambapo mbali na kuishukuru serikali kwa kuwaamini na kuwapa kazi hiyo ameahidi kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kama wanavyotekeleza miradi kama hiyo katika maeneo mengine huku akiwaomba ushirikiano wananchi ili waweze kuikamilisha kazi hiyo kwa wakati
Bi Sarah Michael na Asteria John ni wananchi wa kata ya Buzuruga ambapo wameishukuru serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo kwani wamekuwa wakipata changamoto kubwa katika usafiri pamoja na kero ya vumbi kwa wafanya biashara wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa barabara hiyo huku wakimpongeza mbunge wao kwa kuomba fedha za ujenzi wa mradi huo kutoka serikali kuu
Mbunge wa Jimbo la Ilemela alipata fursa ya kukagua miradi inayotekelezwa ndani ya kata ya Buzuruga, alifanya mkutano wa kusikiliza kero za wananchi wa kata hiyo pamoja na kuwahamasisha kujiandikisha katika daftari la mkazi na kushiriki uchaguzi wa serikaki za mtaa akiambatana na wataalam wa manispaa ya Ilemela na wakuu wa taasisi zinazofanya kazi ndani ya wilaya hiyo ikiwemo Tanesco, MWAUWASA na TARURA