Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, amepongeza maendeleo ya ujenzi wa barabara inayounganisha Bulyanhulu na Kahama baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo muhimu kwa uchumi wa eneo hilo.
Akiwa kwenye ziara hiyo, Mheshimiwa Iddi alieleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi pamoja na ubora wa kazi inayotekelezwa. Aidha, alimshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuboresha miundombinu nchini, hususan katika Jimbo la Msalala.
Mbali na hilo, Mheshimiwa Iddi alitoa shukrani kwa wadau mbalimbali wakiwemo Mgodi wa Bulyanhulu kwa mchango wao muhimu katika kufanikisha ujenzi wa barabara hiyo. Vilevile, aliipongeza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Barabara hiyo inayojengwa inatarajiwa kuboresha usafiri na uchukuzi kati ya Bulyanhulu na Kahama, hatua ambayo itachangia kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi wa maeneo hayo.