Na.Mwandishi Wetu -Arusha
Jumla ya Shilingi Bilioni 1.5 imetengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Kampasi ya Tengeru iliyopo Mkoani Arusha kupitia ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na Poland.
Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kutembelea kampasi hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema serikali inaendelea na upanuzi wa LITA katika kampasi zote nchini ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi soko la ajira.
“Mradi huu ni mmoja ila kuna miradi mingine midogo midogo minne, mradi wa kwanza ulikuwa ni ujenzi wa sehemu ya kukamulia maziwa kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi ambao wapo chuoni hapo, mradi wa pili ni malisho ambao utakuwa wa umwagiliaji na upo katika hatua za mwisho ambapo muda sio mrefu tutaanza uzalishaji wa uhakika na wafugaji watapata chakula cha mifugo yao na mradi wa nne ni vifaa vya Maabara.” Amesisitiza Prof. Shemdoe
Aidha, amesisitiza kuwa mradi wa tatu ni ujenzi wa darasa kubwa ambalo litatumika kwa ajili ya vijana kufundishwa uchakataji wa maziwa.
Pia, amesema kuwa wizara inaishukuru Serikali ya Poland na pia miradi hiyo ni matokeo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Diplomatsia ya Uchumi ya kuendelea kufungua nchi katika nyanja mbalimbali.
Ameongeza kuwa Serikali ya Poland itatoa kiasi cha Shilingi Bilioni Moja na Serikali ya Tanzania itachangia kiasi cha Shilingi Milioni 500.
Hata hivyo katibu mkuu huyo amesema kuwa matarajio ya wizara ni kuona thamani halisi ya fedha inaonekana mpaka kukamilika kwa miradi hiyo.
“Hapa tunatoa Astashahada ya Mifugo kwa wanafunzi wa nje na kuna kozi fupi fupi kwa wafugaji sio wa Tengeru tu hata maeneo mengine, hivyo wafugaji mbalimbali watanufaika na teknolojia hiyo na faida kubwa ambayo itapatikana ni ujuzi na uzoefu kwa watanzania ambao ni wengi kwenye mradi huo.” Amesema Prof. Shemdoe
Kwa Upande wake Mtendaji Mkuu wa LITA Dkt. Pius Mwambene amesema katika kipindi hiki cha awamu ya sita serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni Sita, ambapo fedha hizo zimejenga kumbi nne za mihadhara, zimechangia ukarabati wa maabara zilizopo chuoni hapo, mradi mpya wa jengo la wanafunzi kulala (hostel) chuoni hapo yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 216 kwa wakati mmoja.
Dkt. Mwambene amesema kuwa fedha zimeshapitishwa na serikali ya awamu ya sita wanategemea zikitoka fedha za awali mkandarasi aanze kazi mara moja, vile vile Mwaka 2024 kupitia serikali ya awamu ya sita wametengewa kiasi cha Shilingi Bilioni Tatu kutoka Benki ya Dunia ambapo itasaidia kukarabati Kampasi ya LITA Tengeru na Morogoro kwa kuwa miundombinu yake imekuwa chakavu kutokana na kujengwa mwaka 1702.
Ushirikiano wa Serikali ya Poland na LITA Kampasi ya Tengeru ni kutokana na uwepo wa makaburi ya raia wa Poland ambao walifia eneo hilo wakiwa katika vita ya pili ya dunia ushirikiano kati ya pande hizo mbili ulianza rasmi Mwaka 2009.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (kushoto) akikagua moja ya vifaa vya umwagiliaji kwenye shamba la malisho la Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Kampasi ya Tengeru iliyopo Mkoani Arusha, ambapo Serikali ya Poland kwa kushirikiana na Tanzania inafanya maboresho katika shamba hilo kwa kufunga vifaa vya kisasa kwa ajili ya umwagiliaji. Pembeni yake ni Mtendaji Mkuu wa LITA Dkt. Pius Mwambene.
Muonekano wa moja ya majengo yanayokarabatiwa na Serikali ya Poland kwa kushirikiana na Tanzania katika Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Kampasi ya Tengeru iliyopo Mkoani Arusha, ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe (wa tatu kutoka kushoto) amekagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu katika kampasi hiyo.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akiwa amekaa katika
moja ya madarasa ya Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA)
Kampasi ya Tengeru iliyopo Mkoani Arusha, yaliyojengwa kwa ufadhili wa
Serikali ya Poland ambapo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan namna anavyofungua nchi kupitia
Diplomasia ya Uchumi.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akipata maelezo kutoka kwa baadhi ya wanafunzi wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Kampasi ya Tengeru iliyopo Mkoani Arusha, wakati alipotembelea kampasi hiyo kujionea vifaa mbalimbali vya maabara vilivyotolewa na Serikali ya Poland.