Na. Mwandishi Wetu
Uboreshaji
wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Zanzibar utafanyika kwa siku saba
kuanzia tarehe 07 hadi 13 Oktoba, 2024 ambapo vituo vitafunguliwa saa
02:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Akifungua mkutano wa
wadau wa uchaguzi Kisiwani Pemba, Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa (Mstaafu), Mbarouk
Salim Mbarouk amesema uboreshaji huo wa daftari utajumuisha mikoa ya
Mjini Magharibi, Unguja Kaskazini, Unguja Kusini, Pemba Kaskazini na
Pemba Kusini.
Jaji Mbarouk amesema uboreshaji huo ambao
unafanyika kwenye mzunguko wa sita kwa mujibu wa kalenda ya Tume kwa
upande wa Zanzibar utahusu kuwaandikisha watanzania wote wanaoishi
Zanzibar ambao wanastahili kuandikishwa kuwa wapiga kura kwa ajili ya
uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Akizungumza wakati
akifungua mkutano kama huo Kisiwani Unguja, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa
ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari
ameongeza kuwa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(2) cha Sheria
ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024, Tume
itawaandikisha watanzania waliopo Zanzibar ambao wametimiza umri wa
miaka 18 na zaidi au watakaotimiza umri huo wakati au kabla ya tarehe ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Amefafanua kuwa mtanzania huyo
atakeyandikishwa ni lazima awe hajapoteza sifa kwa mujibu wa sheria ya
uchaguzi au sheria nyingine yeyote na awe anastahili kuandikishwa kuwa
mpiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
“Kwa
lugha nyepesi ni kwamba, Tume itamwandikisha mtanzania yeyote aliyopo
Zanzibar ambaye amekosa sifa za kuandikishwa na Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC). Hivyo, atakayeandikishwa kwenye Daftari la Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi atapiga kura moja tu ya kumchagua Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,” amesema Jaji Asina.
Uzinduzi wa uboreshaji
wa Daftari ulifanyika tarehe 20 Julai, 2024 mkoani Kigoma na mpaka sasa
uboreshaji umeshafanyika kwenye mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Geita,
Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Singida na sehemu ya
mkoa wa Dodoma.
Mjumbe
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari
akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa Wadau wa Uchaguzi katika kisiwa cha
Unguja, Zanzibar leo Septemba 30, 2024 ambapo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
imekutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi kuwapa taarifa juu ya uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotaraji kufanyika Visiwani Zanzibar kuanzia
Oktoba 7 hadi 13, mwaka huu. (Picha na
INEC).
Wadau
wa uchaguzi kutoka vyama vya Siasa, Makundi maalum ya Wanawake, vijana, watu
wenye Ulemavu, Wazee wa Kimila, Wahariri wa vyombo vya Habari wakishiriki
katika mkutano wa Tume na Wadau wa uchaguzi uliofanyika leo Septemba 30, 2024 katika
kisiwa cha Unguja Zanzibar ikiwa ni maandalizi kuelekea zoezi la uboreshaji wa
daftari la Kudumu la Wapiga Kura visiwani Zanzibar ambalo linataraji kuanza Oktoba
7 hadi 13, mwaka huu. (Picha na INEC).