Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb) ameweka jiwe la msingi la Ujenzi wa maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ya Naliendele ambayo itafanya tafiti za kukabiliana na magonjwa ya mimea (parholojia), tarehe 30 Septemba 2024 mkoani Mtwara.
Akiongea na Watumishi wa TARI – Naliendele, Waziri Bashe amewapongeza kwa kufanya kazi kwa kujituma licha ya tafiti na gunduzi zao za mbegu bora kutumika bila kuwa na mfumo wa “royalty return” yaani fidia ya kazi zao.
“Ni jambo ambalo ni la kulifanyia kazi ili angalau kuwe na kitu kidogo cha “royalty return” kipatikane kwa zile gunduzi zilizofanyika, ijapokuwa zimetumia rasilimali za Serikali. Tutaona nini kifanyike,” amesema Waziri Bashe.
Kituo cha TARI Naliendele ni miongoni mwa vituo 17 vya TARI, chenye jumla ya hekta 3151.32 za matumizi ya tafiti mbalimbali. Kituo hicho awali kilikuwa na ekari 165 kwa uzalishaji wa tani 100; ambapo kwa sasa kimeongeza eneo la uzalishaji huo hadi ekari 363 ambazo zitakuwa na uwezo wa kuzalisha mbegu tani 220.
Chini ya uongozi wa Mkurugenzi Dkt. Geradina Mzena, Kituo cha TARI Naliendele kina wataalamu wanaofanya tafiti za mazao ya kimkakati ya Korosho, Ufuta na Karanga, pamoja na mazao mengine yakiwemo ya mboga mboga (horticulture), muhogo na jamii ya mikunde.
Kupitia zao la Korosho, watafiti wa Kituo hicho wameelekeza kuwa tafiti zao zimewezesha ugunduzi wa mbegu kinzani dhidi ya magonjwa, utafiti wa mbolea kwa matumizi ya zao la korosho, ugunduzi wa mbegu zinazozaa au kukomaa mapema; ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa mvinyo kwa kutumia bibo (tunda la korosho).
Ujenzi wa maabara utaongeza wigo wa ufanisi wa kazi za tafiti katika Kituo hicho pia kinatoa hudumia kwa Vituo vya TARI Kifyulilo – Iringa na TARI Kihinga – Kigoma.