Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewahimiza wenye viwanda na kampuni kuhakikisha wanasajili bidhaa zao ili waweze kuzitangaza katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Wito huo umetolewa na Ofisa Leseni wa BRELA, Ndeyanka Mbowe, wakati akizungumza Oktoba 1, 2024, kwenye Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Viwanda nchini yaliyofanyika viwanja vya Sabasaba, Jijini Dar es Salaam.
Mbowe alieleza kuwa lengo la BRELA ni kutoa huduma za usajili wa viwanda na biashara, huku pia wakitoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kusajili bidhaa zao. Huduma hizo zilitolewa katika banda la BRELA kwenye maonesho hayo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo katika kuwafikia wafanyabiashara na wazalishaji wa viwanda.
“Toka mwaka 2018, BRELA imekuwa ikisajili viwanda na kampuni kwa njia ya kisasa, ambapo tumeanza kutumia mfumo wa kidijitali. Hivi sasa wenye viwanda na kampuni wanasajili bidhaa zao mtandaoni kwa urahisi zaidi,” alisema Mbowe.
Alibainisha kuwa BRELA imeweka mikakati madhubuti ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu faida za kusajili kampuni au viwanda. “Ukitengeneza bidhaa na kusajili kampuni yako, unapata fursa kubwa ya kushiriki maonesho ya ndani na nje, ambayo yanatoa nafasi nzuri ya kutangaza bidhaa zako,” aliongeza.
Mbowe pia alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda kusajili bidhaa zao ili kujenga mazingira bora ya kibiashara, akisisitiza kuwa kuna mwitikio mdogo kwenye maonesho hayo, ingawa alihimiza wadau kuendelea kusajili na kushiriki kwa wingi katika maonesho ili kupata elimu na kubadilishana uzoefu.
Mtandao wa habari wa Fullshangwe ulishuhudia baadhi ya wananchi wakifika katika banda la BRELA kupata elimu kuhusu usajili wa viwanda vidogo, vya kati, na vikubwa, huku wengi wakionesha kuridhika na huduma walizopata. Godwin Claudi, mmoja wa waliotembelea banda hilo, alisema: “Leo nimeelewa kazi za BRELA kupitia elimu niliyoipata. Hii imenivutia kuanzisha kiwanda kidogo kwa sababu si ghali kusajili, na nikisajili, nitapata fursa nyingi za kutangaza bidhaa zangu.”
Plakseda Luis, ambaye tayari anamiliki kiwanda kidogo, alikiri kuwa biashara yake haikuwa inaendelea vizuri kwa sababu hakuisajili. “Nilipopata elimu kutoka BRELA, niliweza kusajili biashara yangu, na sasa ninashiriki maonesho mbalimbali kwa lengo la kutangaza bidhaa zangu,” alisema.