Serikali imeidhinisha ujenzi wa kilomita 40 za barabara ya Musoma-Makojo-Busekela yenye urefu wa kilomita 90, baada ya ombi la Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake Mkoani Mara.
Akizungumza katika ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) katika Kijiji cha Suguti, Prof. Muhongo alisema kuwa kwa sasa kinachosubiriwa ni kupatikana kwa mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo.
“Tumepewa kilomita 40 za ujenzi na serikali tayari imetoa tangazo la kumtafuta mkandarasi kwa ajili ya barabara hii. Tunapaswa kupongeza uamuzi huu wa serikali,” alisema Prof. Muhongo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Simbachawene, alipongeza utekelezaji wa miradi katika Mkoa wa Mara na alisisitiza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha inawahudumia wananchi kwa ufanisi kupitia miradi hiyo ya maendeleo.