Mkuu wa Wilaya ya Nyamaga Amina Makilagi akipanda mti kwenye eneo la chanzo Cha maji Butimba
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Butimba wakishiriki zoezi la upandaji wa miti katika chanzo cha maji Butimba kilichopo Wilaya ya Nyamagana Mkoani.
Mwanza.
Mwanamuziki kutoka Mwanza H- Baba akipanda mti kwenye chanzo cha maji Butimba
………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Miche ya miti mbalimbali ambayo ni rafiki katika vyanzo vya maji imepandwa kwenye chanzo cha maji Butimba kilichopo Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza kwa lengo la kuendelea kukilinda.
Hayo yamebainishwa leo Jumanne Octoba 1, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kuongoza zoezi la kupanda miche hiyo.
Amesema kila mmoja awe kielelezo katika utunzaji wa mazingira kwa kulinda na kuitunza miti inayopandwa katika taasisi za umma na kuhakikisha inakuwa.
“Leo tumepanda hii miti hapa kwenye chanzo cha maji na mwenge wa uhuru utakapofika kwenye Wilaya yetu ya Nyamagana utakagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na upandaji wa miti katika hivyo zoezi hili tulilolifanya leo tumetekeleza kauli mbiu ya mbio za mwenge 2024 ambayo inasema’Tunza mazingira shiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa kwaujenzi wa Taifa endelevu’,”amesema Makilagi
Kwa upande wake Kaimu Afisa Maliasili na Mazingira Jiji la Mwanza, David Joseph amesema upandaji wa miti unahifadhi mazingira hususani katika kupunguza hewa ya ukaa.
Naye Afisa Uhifadhi Mwandamizi kutoka wakala wa huduma za mistu (TFS) Wilaya ya Nyamagana, Emmanuel Mgimwa ametoa rai kwa wananchi kuendelea kupanda miti kwaajili ya utunzaji wa mazingira.
Amesema kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 wanatarajia kutoa bure kwa jamii zaidi ya miche ya miti 300,000 ikiwemo ya matunda,kimvuli na urembo.
“Miti hii tutakayoitoa inatakiwa kutunzwa ili thamani ya pesa ya Serikali inayotumika kugharamia miche hiyo iweze kuonekana”, amesema Mgimwa.