Naibu Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Ujenzi, Dk. Charles Msonde, ametembelea Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) katika ziara ya kujifunza na kufahamiana na watumishi wa baraza hilo, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano na uongozi bora. Ziara hiyo ilifanyika katika ofisi za NCC zilizopo Njedengwa, Dodoma, ambapo Dk. Msonde alikutana na menejimenti ya baraza hilo, inayoongozwa na Mtendaji Mkuu, Dk. Matiko Mturi.
Wakati wa ziara hiyo, Dk. Msonde alitembelea kila ofisi ndani ya NCC, akipata fursa ya kusalimiana na kufahamiana na watumishi wa baraza hilo. Pia alifanya kikao kifupi na menejimenti, ambapo Dk. Mturi alieleza kuhusu uanzishwaji wa NCC, majukumu yake, mikakati ya kufikia malengo, pamoja na changamoto zinazolikabili baraza hilo.
Dk. Msonde aliipongeza NCC kwa mchango wake katika Sekta ya Ujenzi, akilitaja baraza hilo kama ‘Think Tank’ ya sekta hiyo. Alisema: “Wizara inawaamini NCC kama chombo chake cha kufikiri. Hongera! Licha ya changamoto mlizonazo, bado mnafanya kazi nzuri.” Aidha, aliitaka NCC kufikiria zaidi namna ya kuwawezesha wakandarasi wazawa kushiriki kikamilifu katika miradi ya ujenzi, akisisitiza kuwa ni muhimu kuwapa nafasi ili waonyeshe uwezo wao.
Dk. Msonde alionya dhidi ya dhana potofu zinazowahusu wakandarasi wa ndani, akisema kuwa wanapewa nafasi na rasilimali zinazohitajika, wataweza kutekeleza miradi kwa ufanisi.
Katika kikao hicho, Dk. Msonde aliagiza NCC kuchambua maandiko mbalimbali yanayohusu sekta ya ujenzi ili kubaini kama kuna vipengele vinavyowazuia wakandarasi wa ndani kushiriki katika miradi mikubwa. Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa NCC kuishauri wizara ili kuondoa vipingamizi hivyo, akisema: “Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inataka wakandarasi wazawa wanufaike na miradi ya ndani.”
Akimazia hotuba yake, Dk. Msonde alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na ubunifu kati ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi. Alisema kuwa ushirikiano huo utasaidia kufanikisha malengo ya taasisi hizo kwa faida ya wote.