Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari leo Oktoba 1, 2024 jijini Dar es Salaam.
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Lulu Mengele akizungumza jambo katika mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari na uongozi wa mfuko huo uliofanyika leo Oktoba 1, 2024 jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF) na Afrika Mashariki Deodatus Balile akizungumza jambo katika mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari na uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliofanyika leo Oktoba 1, 2024.jijini Dar es Salaam.
Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika Mkutano na Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba uliofanyika leo Oktoba 1, 2024.
Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Bw. Masha Mshomba akitoa vyeti vya pongezi kwa vyombo vya habari ikiwemo Mwananchi Communication Ltd, ITV, Azam Media Ltd , Jamhuri Media baada ya kutoa michango ya wafanyakazi wao kwa wakati NSSF.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umewataka watanzania kujiunga na mfuko wa sekta isiyo rasmi (National Informal Sector Scheme-NISS) ambao unatoa fursa kwa wanachama kuchangia kuanzia shilingi 30,000 kila mwezi jambo ambalo litasaidia kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Mfuko huo unatoa fursa kwa mwananchi yeyote aliyejiajiri katika sekta isiyo rasmi ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sanaa mbalimbali, biashara ndogo ndogo, mama lishe au baba lishe, bodaboda, machinga pamoja na wanahabari wa kujitegemea na kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki, mwezi, muhula au msimu.
Akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari leo Oktoba 1, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu NSSF Bw. Masha Mshomba, amesema kuwa NSSF imefanikiwa kupiga hatua kubwa za utendaji ikiwemo kuboresha mifumo ya teknolojia pamoja na kukuza mtaji kwa asililimia 70 kutoka shilingi trillion 4.8 kwa mwaka 2021 hadi kufikia trillion 8.5.
Mshomba amesema kuwa mfumo wa teknolojia umewasaidia wanachama wa NSSF kupata taarifa kwa wakati wakiwa mahali popote pamoja na kuondoa usumbufu uliokuwepo awali.
“Lengo ni kuwafikia watu wengi katika sekta binafsi pamoja na sekta isiyo rasmi, tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suruhu Hassani kwa kutupa ushirikiano katika kuendeleza mfuko wa NSSF” amesema Mshomba.
Akizungumzia huduma ya sekta isiyo rasmi, Mkurugenzi Uendeshaji NSSF, Omary Rufia, amesema kuwa huduma hiyo imelenga kuwasaidia wafanyabiashara wadogo nchini.
“Tutaendelea kutoa elimu kwa jamii ili waweze kujiunga na mfuko huu na kunufaika kiuchumi katika maisha yao pamoja na kusaidia juhudi za Serikali za kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi” amesema Rufia.
Amesema kuwa wamejikita kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa makundi ambayo hayanufaiki na huduma za NSSF ingawa wanashiriki kikamilifu kuchangia uchumi wa Taifa.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF) na Afrika Mashariki Deodatus Balile, ameipongeza NSSF kwa kuboresha utendaji wa majukumu ikiwemo mifumo ya teknolojia ya kutoa taarifa kwa wanachama.
Balile amesema kuwa NSSF imefanya kazi kubwa katika kuboresha utendaji kazi, huku akitoa wito wa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ili kulisaidia Taifa na kupiga hatua kimaendeleo.
“NSSF mnatakiwa kuanzisha ajenda za msingi za utekelezaji wa miradi ya kisasa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, kama mlivyotekeleza mradi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni ambao umekuwa na manufaa makubwa kwa watanzania” amesema Balile.
Wakizungumzia umuhimu wa kujiunga na NSSF Wahariri wastaafu akiwemo Bakari Machumu pamoja na Flora Wingi, wamesisitiza umuhimu wa kujiunga na mfuko huo kwani unamanufaa mazuri baada ya kustaafu kwa kuwasaidia kuishi maisha rafiki lenye kuleta tija katika uchumi.
Katika mkutano huo NSSF wametoa vyeti vya pongezi kwa vyombo vya habari Mwananchi Communication Ltd, ITV, Azam Media Ltd , Jamhuri Media kwa kutoa michango ya wafanyakazi wao kwa wakati.
Pia wametoa tuzo ya shukrani kwa baadhi ya wahariri ambao wamekuwa wakifanya kazi ya kuhamasisha wahariri wa vyombo vya habari kutochukua fedha za kustaafu mapema ili ziweze kuwasaidia uzeeni.