Akitoa tamko la umoja huo leo Oktoba 1,2024 mbele ya waandishi wa habari jijini Dodoma,Mwenyekiti wa Umoja Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT),akitoa tamko kwa waandishi wa habari leo Oktoba 1,2024 kuhusu kukemea kitendo kilichofanywa na Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) cha kuchoma moto vitenge vyenye picha ya Rais Mhe.Dk. Samia Suluhu Hassan.
….
UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) umekemea vikali kitendo cha utovu wa nidhamu kilichofanywa na Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA) cha kuchoma moto vitenge vyenye picha ya Rais Mhe.Dk. Samia Suluhu Hassan.
Bi. Chatanda amesema kuwa hoja zilizotolewa na BAWACHA walizodai ndio sababu ya kuchoma vitenge hivyo kwani Rais Dk. Samia hakuzitafutia ufumbuzi licha ya kumpatia alipokuwa mgeni rasmi katika Baraza Kuu la BAWACHA lililofanyika Machi nane mwaka huu.
Amezitaja hoja hizo zilizotolewa na BAWACHA kuboresha huduma za afya, kupunguza kodi na tozo kwa wafanyabiashara wadogo, kupunguza gharama za maisha na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Hoja zingine ni kurejesha mchakato wa katiba, kutatua kero ya maji hasa maeneo ya vijijini, kuwaondoa wabunge 19 wa viti maalum wa CHADEMA, kuboresha mfumo wa elimu na kupitiwa upya sheria kandamizi kwa wanawake na watoto.
Aidha Chatanda amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, Rais Dk. Samia amezijibu hoja hizo kwa vitendo kwani kwa upande wa sekta ya afya amewezesha ongezeko la vituo vya afya.
Amefafanua kuwa ongezeko hilo ni kutoka kutoka vituo 8,549 mwaka 2021 hadi vituo 9,693 mwaka 2024 sawa na ongezeko la vituo 1,144.
Kuhusu kupunguza kodi na tozo kwa wafanyabiashara wadogo, amesema Rais Dk. Samia, ameunda kikosi kazi cha mapitio ya mifumo ya kodi nchini.
Akizungumzia hoja ya kupunguza ukali wa maisha, ameeleza kuwa kutokana na kazi nzuri ikiwemo utoaji ruzuku ya mbolea na pembejeo kwa wakulima wakiwemo wanachama wa BAWACHA, matokeo chanya yameanza kuonekana.
Amesema kuwa takwimu zinaonyesha pato kwa kila Mtanzania limeongezeka kutoka sh. milioni 2.37 mwaka jana hadi sh. milioni 2.41 kwa mwaka 2024.
“Kuhusu madai ya serikali kushindwa kutatua tatizo la ajira kwa vijana, serikali ya awamu ya sita imejitahidi kutengeneza fursa za ajira zisizorasmi kupitia uwekezaji katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
“Pia, hatua ya serikali kuboresha mitaala ya elimu itawezesha wahitimu kujiajiri kupitia mafunzo ya amali ni jambo la kuungwa mkono kwa wapenda maendeleo na amani nchini,” alisisitiza.
Vilevile, amesema kuwa Rais Dk. Samia amevunja rekodi ya ujenzi na ukarabati wa barabara vijijini na mijini hali iliyochangiwa na ongezeko la bajeti akitolea mfano ya kutoka sh. bilioni 275 hadi sh. bilioni 710 kwa fedha za ndani.
Hivyo, ametoa rai kwa viongozi wa BAWACHA kutafuta ajenda nyingine na kumwacha Rais Dk. Samia aendelee na kazi ya kuwatumikia Watanzania.
“Waendelee kuthamini hatua ya Rais Dk. Samia kukubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika baraza lao Machi 8 mwaka jana. Ni kitendo cha uungwana, upendo, ujasiri.
“Ameingia katika historia duniani ya kuwa na Rais kutoka Chama tawala kuhudhuria mkutano wa chama cha upinzani, hakika tuzo waliyotoa kwa Dk. Samia alistahili kutunukiwa,” amesisitiza Chatanda