Na. Faraja Mbise, DODOMA MAKULU
Naibu Meya wa Halmashauri Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago amefarijika na kampeni ya upandaji miti inayofanywa na wanariadha wanaotumia baiskeli katika kuzienzi falsafa za Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere ya kupambana na adui wa maendeleo kwa kuondoa ujinga, maradhi na umasikini.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akimkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa, Kaspar Mmuya katika zoezi la upandaji miti na ugawaji madawati katika Shule ya Msingi Dodoma Makulu, jijini Dodoma lililofanywa na wanariadha kutokea Dar es Salaam wakielekea Butiama.
Chibago alisema kuwa amefarijika sana na kampeni ya wanariadha hao wa kuendesha baiskeli, upandaji miti ikiwa ni falsafa moja wapo ya kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere katika falsafa zake tatu za kupambana na maadui wa maendeleo ambao ni ujinga, umaskini na maradhi. “Jiji la Dodoma tumefarijika sana na kampeni ya hawa ndugu zetu wanayoendelea nayo pamoja na wadhamini. Wamefanya kitu kizuri sana, nimeona kuna zoezi la kupanda miti. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Makamu wa Rais, wanatamani Dodoma iendelee kuwa ya kijani” alisema Chibago.
Adha, aliwashukuru wanariadha kwa mchango wao wa madawati 100 kwa Shule ya Msingi Dodoma Makulu ambayo yatapekea wanafunzi kukaa na kusoma kwa uhuru zaidi ili kuboresha elimu yao. “Madawati yatawafanya watoto wetu wakae vizuri na kusoma kwa uhuru zaidi” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Dodoma Makulu, Mwl. Amon Sebyiga alitoa shukrani kwa wanariadha na wadhamini kwa kuweza kutatua changamoto iliyokuwepo shuleni hapo ya upungufu wa madawati hali ambayo ilipelekea wanafunzi kukaa zaidi ya watano katika dawati moja. “Tunapenda kutoa shukrani zetu kwa hawa ndugu zetu wa Twende Butiama kwa kutupatia msaada wa madawati 100 ambayo tutakabidhiwa hivi punde. Idadi hii itaenda kupunguza mbanano mkubwa wa wanafunzi darasani” alisema Mwl. Sebyiga.
Wakati huohuo, Mwalimu wa Shule ya Msingi Dodoma Makulu, Denis Thadey alipongeza wanariadha na wadhamini wa madawati shuleni hapo kwa mchango wao mkubwa kwa kuondoa changamoto iliyokuwapo hapo shuleni kwa muda mrefu. Changamoto hiyo ilipelekea wanafunzi kubanana katika dawati moja na hivyo kukosa uhuru wa kusoma nakuandika vizuri. “Nimefurahishwa na tukio hili la wenzetu ambao wameamua kuendesha baiskeli kutoka Dar es Salaam kwenda Butiama kwa ajili ya kuenzi kumbukizi ya Mwl. Nyerere. Ujio wao umekuwa wa mafanikio makubwa sana katika shule yetu. Wametusaidia kuondoa changamoto tuliyokuwanayo shuleni kwa muda mrefu, wanafunzi walikuwa wanasomea chini, lakini kwa kushirikiana na wadhamini Vodacom na Stanbic Bank tumeona msaada wao na moyo wao wa upendo” alisema Mw. Thadey.
Nae mwanafunzi wa Shule ya Msingi Dodoma Makulu, Christian Samson aliipongeza serikali kwa misaada ambayo wanaendelea kutoa shuleni hapo kwasababu inawasaidia katika kukuza taaluma shuleni hapo. “Serikali haituachi nyuma, tumefurahia sana madawati na tunashukuru kwa umoja wenu” alisema Samson.
Zoezi hili la upandaji miti na ugawaji madawati 100 kwa Shule ya Msingi Dodoma Makulu, lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na mashirika binafsi kama Vodacom na Benki ya Stanbic na wanariadha wa msafara wa baiskeli uitwao “Twende Butiama” kutokea Dar es Salaam kwenda Butiama kwa udhamini wa Vodacom na Benki ya Stanbic kwa lengo la kumuenzi Baba wa taifa katika falsafa yake ya kupambana na maadui wa maendeleo na kugawa madawati zaidi ya 1,000 kwa shule shule 13, kupanda miti zaidi ya 50,000, kukabidhi vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kuendesha kambi za afya kwa mikoa mitano ikiwemo Dodoma.