Na Ashrack Miraji – Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Kubecha, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Mhe. Kubecha alisisitiza umuhimu wa wananchi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na kutumia haki yao ya kuchagua viongozi bora watakaoleta maendeleo.
“Nitumie fursa hii kuwasihi wananchi wa Tanga tujitoe kwa wingi kujiandikisha na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu muhimu. Uchaguzi huu ni nafasi ya kuchagua viongozi watakaokuwa chachu ya maendeleo katika wilaya na mkoa wetu wa Tanga,” alisema Mhe. Kubecha.
Aidha, aliwahimiza waandishi wa habari kuendelea kutoa taarifa kwa umma na kuandaa vipindi vya kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa uchaguzi huu. “Tunapaswa kuchagua viongozi wenye uelewa na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya,” aliongeza.
Mhe. Kubecha pia alisisitiza ushirikiano wa viongozi wa serikali katika kuwahamasisha wananchi kushiriki kwenye uchaguzi, huku akitaja kauli mbiu ya mwaka huu: “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi. Jitokeze Kushiriki Uchaguzi.”