Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amewatoa hofu wananchi wa kata ya Shibula kuwa hakuna mwananchi mwenye haki ya kulipwa fidia ya eneo lake litakaloathirika kutokana na ujenzi wa barabara mpya ya kutoka uwanja wa ndege kuelekea Nyanguge wilayani Magu bila kulipwa haki yake
Hayo ameyasema wakati wa mkutano wake wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi katika viwanja vya Mhonze ambapo amesema kuwa Serikali imekwisha tenga fedha kwaajili ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo ilikuwa kero kwa muda mrefu kwa wananchi wa eneo hilo hivyo kuweka vizuizi na ukwamishaji usio na msingi ni kutowatendea haki wananchi wengine
‘.. Tulikuwa na kero ya muda mrefu ya ukosefu wa barabara sasa serikali ya Dkt Samia imetuletea fedha tujenge wapo wenzetu wengine nasikia wanaenda mahakamani, Sasa sijui huko wanafata nini?, Niwahakikishie hakuna mwenye haki atakaekosa stahiki yake ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amewaasa wananchi hao kushiriki katika shughuli za maendeleo pamoja na kujitokeza katika kujiandikisha kwenye daftari la uchaguzi wa serikali za mtaa kwa mwaka 2024 na kilele cha mbio za Mwenge wa uhuru mkoani Mwanza viwanja vya CCM Kirumba
Kwa upande wake mkuu wa idara ya mipango kutoka wakala wa barabara mkoani Mwanza TANROADS Mhandisi Magesa Mwita amesema kuwa upembuzi yakinifu wa barabara ya kutoka uwanja wa ndege kuelekea Nyanguge ulifanywa na mzabuni wa barabara hiyo na baadae wao kama taasisi waliurudia upya ili kuondoa malalamiko na kutenda haki kwa wananchi hivyo kuwahakikishia kuwa hakuna uonevu wowote uliofanyika na kama kutakuwa na malalamiko mengine wapo teyari kukaa meza moja na walalamikaji kwaajili ya suluhu sanjari na kusisitiza kuwa wamefuata sheria na taratibu za ujenzi huo na kuwa kila mwananchi mwenye haki ya kulipwa atalipwa kabla ya kuvunjwa kwa nyumba yake
Mhe Renatus Babehe Mulunga ni mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela mbali na kuishukuru serikali ya Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya manispaa yake, amewataka wananchi wa kata hiyo kuendelea kushirikiana na serikali kupitia sera ya manispaa hiyo ya utatu kwa maana ya wananchi kuibua miradi na kuanza kuutekeleza, mbunge kutoa tofali za ujenzi wa mradi huo na kisha serikali kupitia manispaa kumalizia mradi huo
Sedekia Pamba na Malila Paulo ni wananchi wa mtaa wa Mhonze kata ya shibula ambapo kwa nyakati tofauti katika mkutano huo wamelalamikia zoezi la uwekaji wa alama za uvunjaji nyumba kupisha ujenzi wa barabara bila kuwa na elimu ya kutosha na changamoto za zoezi la upimaji shirikishi
Mbunge Dkt Angeline Mabula anaendelea na ziara za kusikiliza kero za wananchi, kukagua miradi ya maendeleo na kuhamasisha uandikishaji wa daftari la uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na mbio za Mwenge akiambatana na wakuu wa taasisi zilizopo ndani ya wilaya hiyo kama TANESCO, MWAUWASA, TARURA pamoja na wakuu wa idara za manispaa ya Ilemela