Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Salum Ramadhan Abdalla akizungumza na Wafanyakazi wa Idara hio kujitambulisha na kupokea maoni mbalimbali ya kuboresha zaidi utendaji kazi hafla iliofanyika Ofisini kwao Rahaleo Zanzibar.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Idara Habari Maelezo wakimsikiliza Mkurugenzi wao Salum Ramadhan Abdalla katika kikao cha kujitambulisha na kupokea maoni mbalimbali ya kuboresha zaidi utendaji kazi hafla iliofanyika Ofisini kwao Rahaleo Zanzibar.
Na Ali Issa Maelezo
Mkurugenzi Idara ya Habari ya Maelezo Zanzibar Salum Ramadhan Abdalla amesema ushirikiano ndio njia bora itakayoweza kuleta maedeleo na ufanisi katika utendaji wa kazi.
Ameyasema hayo huko ofisini kwake Rahaleo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa Idara hiyo.
Amesema mashirikiano hayo, yataweza kufanikisha utendaji wa kazi na kutatua changamoto zilizopo ili kufanyakazi kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali.
“Iwapo tutakuwa na ushirikiano, tutaweza kutatua changamoto zetu kwa wepesi jambo ambalo litatuletea taswira nzuri kwetu sisi wafanyakazi na taasisi kwa ujumla” alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha aliwakumbusha wafanya kazi hao kufuata utaratibu wa utumishi, kufanya kazi kwa bidii na kufuata kanuni na sheria zilizopo.
Alisema kuwa idara hiyo inatekeleza majukumu mengi hivyo wafanyakazi wanawajibu wa kuweka mikakati madhubuti ya kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Vile vile amewataka wafanyakazi hao kuweka kumbukumbu za viongozi, kuandika Makala, Majarida, kutaarisha vipindi mbali mbali na kuelezea wananchi mambo mazuri yanayofanywa na Serikali.
Nao wafanyakazi wa idara hiyo wameahidi kufanyakazi kwa bidii na kutoa ushirikiano ili kuleta mabadiliko katika utendaji.
Hata hivyo wameomba kutatuliwa matatizo yanayowakabili ikiwemo uhaba wa vitendea kazi na kupatiwa stahiki zao ili waweze kufanyakazi kwa ufanisi.