Yatambulisha Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya Sekta Isiyo Rasmi (NISS)
*Sasa mwanachama kufungua madai ya mafao kidijitali ‘online’
*Yaweka kipaumbele cha matumizi ya TEHAMA, zaidi ya asilimia 82% sasa zinafanyika kutumia mifumo
Yatoa Tuzo kwa Vyombo vya Habari vinavyotekeleza vyema sheria ya NSSF, yatambua mchango wa wahariri wastaafu
Na MWANDISHI WETU,
Dar
es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Bw. Masha Mshomba ameanika mafanikio mbalimbali ambayo Mfuko
umeyafanya yenye lengo la kumuondolea kero mwanachama na kumsogezea
huduma huko huko aliko kwa kutumia mifumo ya TEHAMA. Pia ametambulisha
Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS).
Bw.
Mshomba ameeleza mafanikio hayo tarehe 1 Oktoba 2024 wakati akifungua
mkutano wa NSSF na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ulioshirikisha
wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Nchini, uliofanyika katika
ukumbi wa NSSF Mafao House Ilala, Dar es Salaam.
Amesema
wanaipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo
amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya NSSF hasa katika miaka
minne iliyopita ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri na
wanachama katika Mfuko tofauti na kipindi cha nyuma na kupelekea thamani
ya Mfuko kufikia trilioni 8.5 tofauti na trilioni 4.8 wakati alipokuwa
anaingia madarakani.
Bw. Mshomba amesema NSSF inaendelea
kuboresha huduma zake kupitia mifumo ya TEHAMA na sasa shughuli nyingi
za NSSF zinafanyika kupitia mifumo na kuwa mpaka kufikia mwishoni mwa
mwaka huu wa fedha 2024/25, huduma zote muhimu zitatolewa kupitia
mifumo, aidha alifafanua ya kwamba kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya
shughuli za Mfuko zinafanyika katika Mifumo tofauti na asilimia 42 ya
mwaka 2021/22
“Kupitia mifumo ya TEHAMA, NSSF imeweza kuwafikia
kwa ukaribu wanachama na wadau wake ambapo kwa sasa hawalazimika kufuata
huduma ofisini badala yake wanazipata huko huko waliko na hivyo
tumewaondolea adha ya kufuata huduma umbali mrefu,” amesema Bw. Mshomba.
Aidha,
amesema NSSF imezindua mfumo unaomuwezesha mwanachama kufungua madai ya
mafao kwa njia ya mtandao na kuwa lengo ni kumrahisishia mwanachama
kupata huduma karibu zaidi bila ya kufika katika ofisi za NSSF. Pia
Mfumo huu utaondoa kabisa usumbufu kama ulikuwepo na pia utawawezesha
wanachama wetu tunaowahudumia kupata huduma kwa wakati, kwa kuwa mifumo
hii ni wazi na ufuatiliaji unakuwa rahisi.
Kuhusu sekta isiyo
rasmi, Bw. Mshomba amesema Mfuko umechukua hatua mbalimbali kuhakikisha
wananchi wengi wanahamasika kujiunga na kujiwekea akiba, ambapo kwa sasa
unaendelea kutoa elimu kupitia makundi mbalimbali na kuwaeleza faida za
kujiwekea akiba kwa maisha ya sasa na ya baadaye.
Aidha, kuanza
kwa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS), ni
utekelezaji wa mipango mahsusi iliyowekwa na Shirika la Kazi Duniani
(ILO) (Millenium Goals) ambayo pamoja na mambo mengine inataka watu wote
kuwa kwenye hifadhi ya jamii. Mshomba alifafanua kuwa NSSF imeshaweka
mikakati ya kutosha kuwafikia watu wote ikiwa ni kwa makundi na hata
mwananchi mmoja mmoja. Wananchi wote watakaojiunga na NSSF watapata
Mafao na Huduma mbalimbali kama ambavyo wafanyakazi wengine wote
wanapata.
Uwepo wa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta
isiyo rasmi (NISS) utatoa fursa ya kuongeza wigo wa Hifadhi ya Jamii kwa
makundi ambayo hayanufaiki na huduma hizi ingawa wanashiriki kikamilifu
kuchangia uchumi wa nchi, utasaidia juhudi za Serikali za kupunguza
umaskini wa kipato kwa wananchi, utaongeza nguvu za uzalishaji mali na
kukuza uchumi wa Nchi na mwisho utachochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi
kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Bw. Mshomba amesema pia NSSF
ina Skimu ya uchangiaji wa Hiari ambayo inawahusu watumishi wote.
“Natumia nafasi hii kuhamasisha na kuwataka mchangie kupitia skimu hii
kwa sababu kufanya hivyo mtajikuta mnapata kipato cha ziada, kazi kubwa
mbele yetu ni kutoa elimu ili watu wengi wapate uelewa wa jambo hili.”
amesema.
Naye, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Deodatus Balile amepongeza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na NSSF
hasa katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo wa
kukamilisha kiwanda cha sukari Mkulazi. Pia amepongeza NSSF kuweka
mipango sasa ya kuwafikia wananchi wote walioko katika Sekta isiyo rasmi
kwani kwa kufanya hivyo sasa watu wote tutakuwa ni wamoja na hapo
baadaye wote tutanufaika, safari ya uzee ni ya kila mmoja wetu na hivyo
ni vizuri kila mmoja akifika awe na uhakika wa kesho yake.
Balile
alitumia fursa hiyo kuwakumbusha waajiri wa sekta binafsi hasa wamiliki
wa vyombo vya habari kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi
wao NSSF kwa wakati ili wanapostaafu waweze kulipa stahiki zao.
“Leo
tumepata bahati tumepata ushuhuda kutoka kwa wastaafu waliokuwa
wafanyakazi kutoka katika vyombo vya habari ambao ni wanufaika wa mafao
ya kustaafu na pensheni ya kila mwezi Bi. Flora Wingia na Bw. Bakari
Machumu” Aidha, wahariri wastaafu wamepewa Tuzo kwa kutambua mchango
wao.
Akiwasilisha taarifa ya uendeshaji wa Mfuko, Mkurugenzi wa
Uendeshaji, Bw. Omary Mziya amesema NSSF inaendelea kutekeleza majukumu
yake ya msingi ambayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na
sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao.
Bw.
Mziya amesema wanaendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa hifadhi ya
jamii ili kuongeza uelewa wa haki ya kujiunga kwenye Skimu ya Hifadhi ya
Jamii kwa Sekta isiyo rasmi (NISS) na kuendelea kuboresha mifumo na
kusogeza huduma karibu na jamii.
“Sekta isiyo rasmi ina
Watanzania takribani 11 Millioni, hawa wote wanahitaji kinga dhidi ya
majanga ambayo ni uzee na majanga mengine yanayoweza kutokea hapa kati,
kuachishwa kazi ama kufariki na kadhalika”.
Sekta isiyo rasmi
inatoa nafasi kwa Watanzania wote kujiunga na hifadhi ya jamii,
Mwananchi yeyote aliyejiajiri katika sekta isiyo rasmi kama vile kilimo,
ufugaji, uvuvi, uchimbaji mdogo wa madini, sanaa mbalimbali, biashara
ndogo ndogo, mama lishe/ Baba lishe, bodaboda na wasafirishaji wengine,
machinga, wanahabari wa kujitegemea.