NA MWANDISHI WETU, KIBAHA
Jumuiya ya umoja wa wanawake wa Chama cha mapinduzi (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini imeungana na Mwenyekiti wao wa Taifa Mary Chatanda kupinga na kulaani vikali kwa baadhi ya wanawake wanaodaiwa kuwa ni wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema (BAWACHA) kuchoma vitenge ambavyo vilikuwa na picha ya Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hasssan kitendo ambacho sio cha uzalendo katika Taifa la Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutoa tamko juu ya tukio hilo Mwenyekiti wa (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja amesema kwamba wanawake wote kwa umoja wao wamesikitishwa sana kuona vitenge vyenye picha ya Rais vinachomwa hadharani na picha zake kusambaza katika baadhi ya mitandao kitendo ambacho sio cha kiungwana hata kidogo.
Mgonja alibainisha kwamba kitendo hicho ni utovu mkubwa wa nidhamu kwani kufanya hivyo ni ukosefu wa maadili ya nchi na kwamba kundi la wanawake hao wameamua kuvunja heshima baada ya kusema maneno ya uwongo ambayo yanaweza kuleta uchonganishi mkubwa baina ya wananchi pamoja na Rais Samia.
Mwenyekiti huyo alifafanua kwamba Rais wa waamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kufanya mambo makubwa katika miradi mbali mbali ya maendeleo na hivyo maneno ambayo yamesemwa na baadhi ya wanawake hao hayana ukweli kabisa hata kidogo hivyo amewaomba watanzania wote kuwa na uzalendo na nchi yao na kuachana kabisa na maneo ya kashfa kwa Rais Samia.
“Sisi kama Jumuiya ya wanawake wa umoja (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini tunapinga vikali kabisa na kulaani kitendo hicho kilichofanywa hivi karibuni na baadhi ya wanawake wanaodaiwa kuwa wa (Bavicha) kuchoma vitenge vyenye picha ya Rais Samia huu ni ukosefu mkubwa wa utovu wa nidhamu na maadili kwa hivyo jambo hili limetuumiza sana na alipaswi kufumbiwa macho hata kidogo,”alisema Mwenyekiti Mgonja.
Katika hatua nyingine aliviomba vyombo vya dola ambavyo vinahusika na usalama kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wanawake wote ambao wamehusika kwa makusudi kuchoma kitenge chenye picha ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba wangekuwa wazalendo na nchi yao wasingefanya tukio kama hilo ambalo wao kama wanawake hawawezi kulifumbia macho hata kidogo.
Kadhalika alisema kitendo walichokifanya ni uchochezi na ni uvunjifu wa amani hivyo wanapaswa kukamatwa kwani wameshindwa kuheshimu mamlaka na madaraka aliyonayo Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba wameahidi kuendelea kumlinda na kumtetea kwa hali na mali kwani amefanya mambo makubwa kwa wananchi wa Tanzania katika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja naa ili mikubwa ya kimkakati.