Dkt Lazaro Komba akizungumza katika maadhimisho ya kilele Cha elimu ya watu wazima (MEMKWA)
……………..
Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, amepongeza mafanikio ya wanafunzi 282 kati ya 302 waliofanya mitihani ya kitaifa ya upimaji wa darasa la nne kwa mwaka 2023, ambao wamefanikiwa kujiunga na mfumo rasmi wa elimu. Aidha, wanafunzi 1,785 wakiwemo wavulana 899 na wasichana 886, wamejiunga na madarasa ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliokosa (MEMKWA) kutoka halmashauri nne za mkoa huo.
Makongoro Nyerere ametoa pongezi hizo wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku ya Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika Wilaya ya Kalambo, ambako aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Dkt. Lazaro Komba. Katika hotuba yake, Dkt. Komba alisisitiza umuhimu wa jamii kujiendeleza kielimu kwa kushiriki katika programu za elimu ya watu wazima.
Dkt. Komba alibainisha kuwa shule zote mkoani Rukwa zina vyumba maalum kwa ajili ya watu wazima kujiendeleza kielimu. Pia, alieleza kuwa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanaonesha kuwa asilimia 25.9 ya watu wazima hawajui kusoma, kuandika, na kuhesabu (KKK), na kwamba changamoto hiyo inahitaji hatua za dharura.
Pia, Dkt. Komba aliwataka wazazi na walezi kutimiza majukumu yao ya malezi kwa kuhakikisha watoto wao wanahudhuria masomo katika mfumo rasmi wa elimu, ili kuepusha changamoto zinazoweza kukwamisha maendeleo yao.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Rukwa, Matinda Mwinuka, alisema ukosefu wa vitendea kazi maalum kwa ajili ya elimu ya watu wazima na mwamko mdogo wa vijana kujiunga na vyuo vya elimu ya watu wazima ni changamoto kubwa kwa walimu katika kutoa elimu hiyo.
Wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule hizo wameomba serikali kuongeza walimu wenye weledi na maadili ili kusaidia kuboresha viwango vya ufaulu wa wanafunzi. Vilevile, wadau wa elimu mkoani humo, akiwemo Edwin Moses, wamesisitiza umuhimu wa serikali kuwekeza zaidi katika elimu ya watu wazima kwa kuboresha miundombinu na kuongeza vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kufanikisha malengo yao.