OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu ( Afya ) Ofisi ya Rais- TAMISEMI Dkt. Grace Magembe amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa, Halmashauri pamoja na Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za Afya ya Msingi nchini kufanya kazi kwa uadilifu pamoja na kushughulikia changamoto zilizopo katika maeneo yao.
Dkt. Magembe ametoa wito huo alipozungumza na viongozi hao katika kikao kazi kilichofanyika katika viwanja vya maonesho ZIFT vilivyopo Zanzibar .
“Sekta ya afya imeshikiria maisha ya watanzania sasa tufanye kazi tukifuata maadili na misingi ya taaluma zetu , tukishirikiana na mkasimama katika nafsi zenu mtanisaidia mimi kutimiza majukumu yangu,”amebainisha
Aidha, amewataka kushirikiana na watumishi waliopo chini yao pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao huku akisisitiza kuwa moja ya majukumu yao ni kuwasemea watumishi waliopo katika maeneo yao.
“Niwaombe sana kama kuna migongano na changamoto baina yenu zitatueni mapema sisi ni viongozi, kazi yetu kubwa ni kuwasemea watumishi waliopo katika maeneo yetu na sio kuwatengenezea mazingira magumu ya kazi, naumia sana nikisikia watumishi hawaelewani umoja wetu ndio chachu katika kutimiza majukumu yetu tuwe na moyo wa kusaidiana, ” Amebainisha
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambae pia ni Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Mikoa Tanzania Dkt. Honoratha Rutatinisibwa ameahidi maelekezo yaliyotolewa yatatekelezwa ili kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.