Handeni, Tanga
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Mhandisi Mshauri (UWP) pamoja na AFRISA Consulting Limited wameshirikisha wananchi katika zoezi la usanifu wa barabara ya Sindeni – Kwedikwazu Km 38 na Michungwani-Bondo-Kwadoya Km 19 zitakazojengwa kwa kiwango cha lami kupitia mradi wa RISE wilayani Handeni-Tanga.
Zoezi hilo la usanifu wa barabara ulishirikisha makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo akina mama, wazee, vijana na wanafunzi katika vijiji vya Bondo, Michungwani, Kwadoya, Kwamgwe, Ngojoro, Komdudu, Komfungo, Kwamkono, Kwedikwazu, Kwesasu, Mbuyuni, Mumbwi, Mzundu, Sezafoki na Sindeni.
Mradi wa RISE ni mradi wa Uboreshaji wa Barabara Vijijini kwa Ushirikishaji wa Jamii na Ufunguaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi.
Mradi huu unatekelezwa na TARURA na unagharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia na unatarajia kujenga barabara Km 535 katika mikoa ya Iringa, Tanga, Lindi na Geita.