JOHN BUKUKU, GEITA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema litaendelea kusimamia mikataba ya kimataifa na sheria za usalama majini ili kupunguza au kuondoa vifo vinavyotokea baharini.
Hayo yamesemwa leo, Oktoba 4, 2024, na Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Geita, Godfrey Chegere, wakati wa Maonesho ya Saba ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kwenye Viwanja vya EPZ Bombambili, Geita. Chegere alisema kuwa mkoa huo una vyombo vya majini 2,800 vinavyofanya shughuli za uvuvi.
Chegere alieleza kuwa TASAC imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo hivyo kabla ya wahusika kuanza shughuli zao za uvuvi. Alisisitiza kuwa ni muhimu wadau kufika TASAC kabla ya kuanza shughuli za majini ili kupata ushauri kuhusu aina sahihi ya boti wanayopaswa kutumia ili kufanikisha shughuli zao kwa usalama.
Aidha, alisema kuwa mkoani Geita kuna vyombo vinavyosafirisha abiria kutoka sehemu moja hadi nyingine, na vyombo hivyo vimekuwa vikikaguliwa na kupewa leseni baada ya kufikia viwango vya usalama.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoridhia mikataba ya kimataifa kuhusu usalama wa baharini. Tunahakikisha tunazingatia sheria hizi ili kuondoa vifo vya watu majini,” alisema Chegere.
Pamoja na hayo, aliendelea kueleza kuwa TASAC inaendelea kutoa elimu kwa wadau wa majini kuhusu namna ya kujiokoa wakati wa dharura wanapokuwa majini. Alihimiza wasafirishaji wa mizigo, abiria, na wavuvi kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya kujiokoa kama maboya na vifaa vingine vya kuokolea maisha.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Kitengo cha Ukomboaji wa TASAC, Bw. Jackson Mlela, alieleza kuwa kwa mujibu wa sheria, TASAC inalo jukumu la kufanya shughuli za kiforodha kwa bidhaa tano maalum ambazo zinajumuisha makemikia, kemikali zinazoingia nchini, slaa, nyara za serikali, na wanyama pori walioko chini ya sheria za wanyama pori.