Meneja Oparesheni wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail Zanzibar, Sasikumar Venkatachalam (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kampuni hiyo na wa Kampuni za DNATA wakati walipokuwa wakifanya usafi katika Ufukwe wa Kilimani Zanzibar.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WAFANYAKAZI wa Kampuni za DNATA na Emirates Leisure Retail Zanzibar zinazojishughulisha
na utoaji huduma kwa wageni katika Uwanja mpya wa Ndege Zanzibar (AAKIA) ,wamejitolea
kufanya usafi katika Ufukwe wa Kilimani Zanzibar.
Meneja Oparesheni wa Kampuni ya Emirates Leisure Retail Zanzibar, Sasikumar
Venkatachalam akizungumza wakati wa tukio hilo alisema katika kuunga mkono
jitihada za Serikali za utunzaji wa mazingira kampuni hizo ziliamua kuandaa
siku kwa ajili ya kufanya usafi katika uwanja huo.
“ Pamoja na kutoa huduma kwa wageni katika uwanja huu pia ni wajibu wetu
kuhakikisha mazingira tunayotolea huduma yanakuwa ni masafi na ndio maana tupo
hapa tukifanya usafi,” alisema Venkatachalam.
Alisema kuwa kampuni hizo zimeanzisha utaratibu wa kujitolea kwa jamii kufanya
usafi ili kutunza mazingira yote wanayoizunguka jamii hasa maeneo ya fukwe.
Venkatachalam alisema kazi hiyo ya kufanya usafi itakuwa ni endelevu ambapo
pia watafanya utaratibu wa kuhamasisha jamii kushiriki kwenye kazi hiyo ambayo
ni muhimu katika utunzaji wa mazingira.