Waziri wa Kilimo Husein Bashe akizungumza wakati akizindua kiuatilifu-hai kinachojulikana kwa jina la Thutisave 24 (T-24) kinachozalishwa na Kiwanda cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL) leo Kibaha Mkoani Pwani.
Waziri wa Kilimo Husein Bashe akipewa maelezo katika Kiwanda cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL) kabla ya kuzindua kiuatilifu-hai kinachojulikana kwa jina la Thutisave 24 (T-24) kinachozalishwa kwenye kiwanda hicho leo Kibaha Mkoani Pwani.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Dkt Nicolaus akizungumza wakati wa uzinduzi kiuatilifu-hai kinachojulikana kwa jina la Thutisave 24 (T-24) kinachozalishwa na Kiwanda cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL) leo Kibaha Mkoani Pwani.
Baadhi ya wadau na wafanyakazi wa kiwanda Kiwanda cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL) walioshiriki katika wa uzinduzi kiuatilifu-hai kinachojulikana kwa jina la Thutisave 24 (T-24) ambao umezinduliwa leo na Waziri wa Kilimo Husein Bashe katika kiwanda hicho Kibaha Mkoani Pwani.
…………………….
MUSSA KHALID,KIBAHA PWANI
Waziri wa Kilimo Husein Bashe amesema serikali ya Awamu ya sita inaendelea na jitihada za kuhakikisha kunakuwa na Taifa lenye chakula toshelevu na jamii zenye afya imara kwa kutumia bidhaa zisizo na kemikali katika mazao
Waziri Bashe ametoa kauli hiyo leo Kibaha Mkoani Pwani wakati akizindua kiuatilifu-hai kinachojulikana kwa jina la Thutisave 24 (T-24) kinachozalishwa na Kiwanda cha Tanzania Biotech Product Limited (TBPL).
Aidha Waziri Bashe amesema kuwa serikali imeendelea kuimarisha matumizi y anjia za kibailojia kwa kuzalisha wadudu rafiki sambamba na kusajili viuatilifu hai kwa ajili ya udhibiti wa wadudu waharifu shambani kama viwavijeshi vamizi.
“Kwa kuwa viuatilifu hai hivi vina uwezo wa kupambana na wadudu dhurifu kwenye korosho, hii ni habari njema kwani itasaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka tani 254,500 mwaka 2023/2024 hadi tani 595,000 katika mikoa ya Ruvuma, Pwani, Lindi, Dodoma, Mtwara na Tanga”amesema Waziri Bashe
Awali akizungumza Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Dkt Nicolaus Shombe amesema kwa mujibu wa takwimu ya mwaka 2021/2022 zinaonyesha kuwa serikali imetumia takriban Shilingi Bill 212 kwneye viuatilifu vya kemikali kupambana na wadudu hivyo kuzinduliwa kwa Thutisave 24 kutasaidia mapambano na wadudu waharibifu.
Dkt Shombe amesema Sampuli iliyozalishwa ilitumika kwa ajili ya majaribio shambani (field trials) yaliyofanywa na Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI kwenye mikoa ya Morogoro, Mwanza, Tabora, Simiyu na Geita. Lengo likiwa ni kuthibitisha ubora wa kiuatilifu hiki kwenye kupambana na wadudu waharibifu wa mazao ya Pamba na Mahindi (Fall Army worm na American bollworm).
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaj Abubakari Kunenge amesema kuwa uwepo wa kiwanda hicho ni moja ya mafanikio ya mkoa huo kwani kitaendelea kuongeza ufanisi katika kukuza uchumi wan chi.
Katika Halfa hiyo imehudhuriwa na mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali akiwemo Balozi wa kiuba nchini Tanzania Yodenis Vera,pia Imeelezwa kuwa Kiwanda cha TBPL kina uwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali za kibinadamu ikiwemo viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu,Mbolea Hai,Virutubisho vya Chakula pamoja na aina mbalimbali za chanjo za wanyama.