Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeshiriki Maonyesho ya 7 ya Madini na Teknolojia yanayofanyika katika Viwanja vya EPZ, Bombambili, mjini Geita. Lengo la kushiriki ni kuwaonyesha Watanzania bidhaa mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo, ikiwa ni pamoja na nyumba za kupangisha, nyumba za kuuza, ukandarasi na miradi ya viwanja wanavyouza.
Akizungumza leo, Oktoba 5, 2024, Afisa Uhusiano wa NHC, Yamlihery Ndullah, amesema kuwa shirika hilo lina nyumba katika mikoa yote ya Tanzania, zikiwemo nyumba za gharama nafuu, zikiwemo zile za mkoani Geita, eneo la Bombambili, pamoja na miradi mingine iliyopo Dodoma katika eneo katika eneo la Iyumbu( Iyumbe Satellite Center) Samia Housing Scheme-Kawe jijini Dar es Salaaam, Ambapo amesema kuwa Samia Housing Scheme ni mradi unaotarajiwa kufikia mikoa mitano ya Tanzania wakianza na Dar es Salaam na Dodoma.
“Vilevile, Shirika la Nyumba la Taifa lina miradi ya maduka tunayopangisha katika maeneo mbalimbali Tanzania kama Zongomela-Kahama, Mtanda-Lindi, Masasi-Mtwara, Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda pia katika mikoa mingine. Pia tuna miradi mikubwa jijini Dar es Salaam, ikiwemo Morocco Square, iliyopo kwenye makutano ya barabara ya Morocco na Kawe711. Vilevile tunauza viwanja katika eneo la Burka-Mateves mkoani Arusha,” amesema Ndullah.
Shirika la Nyumba la Taifa linawakaribisha Watanzania wote kutembelea maonyesho hayo ili kuona na kujadili fursa za kumiliki nyumba zao. Kwa wale watakaoshindwa kuhudhuria, wanahimizwa kufuatilia taarifa kupitia mitandao ya kijamii ya shirika hilo na website ya shirika www.nhc.co.tz
Maonyesho hayo yamefunguliwa leo Oktoba 05,2024 na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu Dotto Biteko na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 13,2024 na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan.