………………
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kanda ya kaskazini imeanza kutoa mafunzo kuhusu maswala ya bima kwa walimu wa shule za sekondari zilizopo kwenye Halmashauri ya Arusha (DC) mkoani Arusha.
Akizungumza katika uotaji wa elimu hiyo kwa walimu wa shule za sekondari zaidi ya 50, Meneja wa TIRA kanda ya kaskazini, Bahati Ogolla yaliyofanyika katika shule ya sekondari Mringa ,amesema kuwa wameanza kutoa mafunzo kwa walimu hao ili waweze kuwa mabalozi wa bima kwa wanafunzi wanaowahudumia.
Amesema kuwa, walimu hao ambao ni mabalozi wa bima kutoka shule zao watasaidia sana kuanzishwa kwa klabu za bima mashuleni ambazo zitasaidia wanafunzi hao kuendelea kutoa elimu ya bima kwa wenzao na hatimaye kupata uelewa huo wakiwa bado wadogo.
Ameongeza kuwa ,baada ya walimu hao kwenda kutoa elimu kwa wanafunzi wao na kuwezesha kuanzishwa kwa klabu hizo kutasaidia sana elimu hiyo kusambaa katika shule mbalimbali kwani wanafunzi hao nao watakuwa chachu kwa wanafunzi wenzao.
“Wanafunzi hawa watakapopata elimu hiyo na kuweza kuanzisha klabu za bima mashuleni kutasaidia sana elimu hiyo kuweza kusambaa zaidi kwa haraka na kuweza kujua umuhimu wa kutumia bima wakiwa tangu wadogo “amesema Ogolla.
Aidha, Meneja amesema kwa kuanzia wameanza na shule za sekondari zilizopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha ambapo walimu hao watapata fursa ya kwenda kuongea na wanafunzi wao na hatimaye kuweza kuwa mabalozi wazuri kwa kuanzisha klabu za Bima ambazo zitatumika kutoa elimu hiyo.
Aidha ameitaka jamii kuchangamkia fursa za bima zilizopo ikiwemo bima za muda mrefu (bima za miasha) na bima za muda mfupi (bima zisizokuwa za Maisha) pamoja na kufahamu wajibu wao wa kutoa taarifa ya ajali /janga kwenye kampuni za bima walipokatia bima pindi ajali inapotokea.
Kwa upande wake Mshiriki katika mafunzo hayo,Mwalimu kutoka shule ya sekondari Kiserian, Upendo Mwakasata amesema kuwa kitendo kilichofanywa na Mamlaka hiyo ni mfano wa kuigwa kwani kinasaidia sana kuwapa uelewa wa kutosha wanafunzi kuhusu maswala ya bima na kazi zinafanywa na Mamlaka hiyo na kuwezesha wanafunzi hao kupata uelewa wakiwa tangu wadogo.
Naye Mwalimu wa shule ya msingi Mringa, Evance George amesema kuwa, kupitia elimu hiyo watahakikisha wanakuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao na kwa wanafunzi wanaowaongoza huku wakihakikisha klabu mbalimbali za bima zinaanzishwa mashuleni na kuzisimamia kwa umakini .