Na Ashrack Miraji – Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, ameipa Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, na Halmashauri ya Same siku saba (7) kuhakikisha mgogoro wa matumizi ya maji kwenye Mfereji wa Umwagiliaji wa Shakaka unatatuliwa. Mfereji huu unahudumia maeneo matano katika Kata za Vuje na Maore, ikiwa ni pamoja na wakazi wa Kitongoji cha Kalung’oyo (Vuje).
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kitongoji cha Kalung’oyo kwa ajili ya kutatua malalamiko ya wananchi, DC Kasilda Mgeni alisisitiza umuhimu wa kuitisha mkutano wa hadhara maalum ili wananchi waweze kuchagua viongozi watakaosimamia shughuli za mfereji huo.
“Watu wa Bonde la Pangani msiondoke bila mpango thabiti. Shirikianeni na Halmashauri na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ugawanyaji wa rasilimali ya maji. Hatuwezi kufikia hali ambapo wananchi hawana maji ya kuoga kwa sababu maji yote yanatumika kumwagilia mashamba,” alisema DC Kasilda.
Wananchi wa Kalung’oyo wameeleza kuwa licha ya uwepo wa miundombinu ya mfereji wa Shakaka, wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya umwagiliaji kutokana na baadhi ya watu kuelekeza maji kwenye maeneo yao binafsi kwa kutumia mipira. Hali hii imepelekea kilio cha wananchi kuomba serikali iingilie kati kutokana na umuhimu wa mfereji huo katika kilimo chao.
Kwa upande wake, Patrice Nyamulo, mwakilishi kutoka Bodi ya Maji Bonde la Pangani, alisema kuwa changamoto kubwa kwenye mfereji huo ni kukosekana kwa vibali rasmi vya matumizi ya maji, hali inayosababisha matumizi holela na migogoro kati ya watumiaji. Alisisitiza kuwa Bodi ina jukumu la kusimamia na kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha matumizi ya maji yanafanyika kwa mujibu wa sheria.
Mfereji wa Shakaka unatoa huduma kwa maeneo ya Kalung’oyo, Vuje, Chenona (Kata ya Vuje), Gwaya na Maweni (Kata ya Maore), yote yakitegemea chanzo cha Mto Hingilili unaopatikana Kata ya Vuje. Usimamizi wa mto huo unafanywa na Bodi ya Maji Bonde la Pangani, yenye makao makuu mjini Moshi.