Mradi wa Afya Yangu Kanda Ya Kusini umetunukiwa tuzo ya utendaji bora wa mpango wa VVU kupitia kampeni yake ya Sahabiki Salama inayotekelezwa huko mkoani Iringa katika tuzo za PEPFAR HIV Best Practice Award 2024 zinazotolewa na PEPFAR wakati wa Mkutano wa 11 wa Kilele wa Afya Tanzania (THS) uliomalizika Zanzibar mwishoni mwa wiki hii.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hizo Mshauri wa Maswala ya Mabadiliko ya Tabia katika Jamii wa Mradi huo, Mohammed Mwenga alisema kuwa ni heshima kutokana na kazi kubwa na dhamira ambayo mradi huo umekuwa ukifanya katika kuboresha afya, ustawi na ulinzi wa yatima, watoto wanaoishi katika mazingira magumu na vijana katika jamii zenye mzigo mkubwa wa VVU.
Mradi wa USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini (2021- 2026) unalenga kusaidiana na Serikali ya Tanzania kutoa huduma bora jumuishi za matunzo, matibabu, na kuzuia maambukizi ya VVU na kifua kikuu ambazo zitaboresha matokeo chanya ya afya, hasa kwa vijana na watoto.
Mradi unakusudia kuongeza mahitaji na matumizi jumuishi ya huduma bora za VVU na kifua kikuu katika mikoa ya Iringa, Lindi, Morogoro, Mtwara, Njombe, na Ruvuma kwa kuboresha upatikanaji wa huduma bora katika vituo vyote vya afya na jamii zote zinazozunguka maeneo hayo, ili kukuza tabia chanya kwa watanzania kupata huduma za afya na kuimarisha mazingira ya jumla ya sera ya utoaji wa huduma za VVU na kifua kikuu. Mradi huu wa USAID Afya Yangu Kusini unafadhiliwa na Msaada Kupitia Watu wa Marekani na kutekelezwa na Deloitte Consulting Limited Pamoja na washirika wake wenza MDH na T-MARC.
Akizungumzia tuzo hizo, Mratibu wa PEPFAR nchini, Jessica Greene alisema PEPFAR pamoja na Tanzania Health Summit waliamua kujumuika pamoja na kuadhimisha mashujaa katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI.
“Tuzo hizi zinalenga kutambua ubora kwa kutambua na kusherehekea mashirika, Vikundi au Watu Binafsi ambao wanaonyesha michango bora katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, kupitia mikakati madhubuti na ya kiubunifu ya programu na afua ambazo zimefanikiwa kufikia au kuboresha matokeo kati ya vijana, wanaume, watoto na. watu muhimu walio katika mazingira magumu” alisema Greene.
Shughuli za PEPFAR zinalenga katika
kupanua upatikanaji wa afua za kuzuia VVU, matibabu na matunzo. Hizi ni pamoja na utoaji wa matibabu ya kurefusha maisha, kinga ya kabla ya kuambukizwa, tohara ya hiari ya wanaume, kondomu, na bidhaa nyingine
zinazohusiana na huduma za VVU.
Tukio hilo la siku tatu litaitisha mfumo mzima wa huduma ya afya, kuunganisha na kuendeleza mahusiano ambayo yanahamisha ajenda ya SDG.