Balozi wa Tanzania nchini Comoro,Saidi Yakubu amekaribishwa rasmi katika mji wa Bangoi Kuoni na kuzungumza na uongozi wa mji huo kuhusu ushirikiano na miji ya Tanzania.
Katika hafla hiyo ambapo wakazi wa mji huo walimvika rasmi ukaazi wa heshima Balozi Yakubu, viongozi wake walimueleza pia kuwa huo umekuwa ni utamaduni wao wa kushirikiana na Mabalozi wa Tanzania nchini Comoro na kumueleza historia ya mji huo na Tanzania hususan Zanzibar na Tanga.
Aidha,walimueleza kuwa viongozi wa Tanzania waliowahi kutembelea mji huo ni pamoja na Marehemu Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi,Rais wa Zanzibar Mstaafu Amani Abeid Karume,Kiongozi wa Upinzani wa Zanzibar,Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na pia kumtajia viongozi kadhaa wa Tanzania wenye asili ya mji huo.
Kwa upande wake,Balozi Yakubu alishukuru kwa kutuzwa Ukaazi wa Heshima na kuwaahidi kuendeleza utamaduni huo na kutekeleza masuala yote yalioahidiwa na Mabalozi waliomtangulia ikiwemo kuwasaidia kuwa na darasa mahsusi la Kiswahili kwa mji huo.
Balozi Yakubu pia alipata fursa ya kutembelea maeneo kadhaa ya vivutio vya mji huo ikiwemo Msikiti wa Maajabu na pia kuona miradi ya maendeleo inayofanywa kwa juhudi za wananchi na pia Serikali.