Na WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameongozana na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama na viongozi mbalimbali toka mkoani Kilimanjaro na Wizara ya Afya na kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Halmashauri ya Moshi iliyopo katika Kata ya Mabogini.
Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kuona maendeleo ya ujenzi, na kuongea na wananchi ambapo kabla ya kwenda Mabogini, ujumbe wa Waziri Mhagama ulitembelea na kukagua Hospitali ya Wilaya ya Manispaa ya Moshi na Shule ya Sekondari ya Mawenzi.
Baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Kata ya Mabogini, Waziri aliridhishwa na Kazi kubwa inayoendelea ambapo Hospitali ya Mabogini imeshaanza kutoa huduma kwa wananchi kwa ngazi ya Zahanati.
Akitoa salamu katika kata ya Mabogini, Mbunge Ndakidemi alimwomba Waziri apeleke shukrani za wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini kwa Rais Samia Suluhu Hasani kwani kwa kipindi cha miaka minne wamepata miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 45.
Mbunge Ndakidemi aliishukuru sana Serikali kwa kuamua kujenga hospitali ya wilaya katika kata ya Mabogini yenye watu zaidi ya elfu 57 kwani kulikuwa na uhitaji mkubwa.
Ndakidemi alimwamhia Waziri kwamba hadi kufikia sasa, serikali imetoa shilingi 1.8 bilioni ambazo zitakamilisha ujenzi awamu ya kwanza utakaohusisha jengo la wagonjwa nje (OPD), jengo la mama na mtoto, jengo la maabara, jengo la mama na mtoto, jengo la kufulia, jengo la utawala, jengo la mionzi na jengo la dawa.
Akiongea na mamia ya wananchi wa Kata ya Mabogini, Waziri Mhagama aliwaeleza wananchi kuwa Serikali imeleta fedha kwaajili ya miradi mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya ambapo fedha zilizoletwa ni kiasi cha shilingi Bilion 129 zitakazoshughulikia Sekta ya Afya katika Halmashauri hiyo.
Amesema, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Kata ya Mabogini ikikamilika itakua na wodi za kulaza wagonjwa pamoja na nyumba za watumishi ili wananchi wasipate tabu pindi wanapotaka kupata huduma za afya hata ikiwa ni usiku.
“Kwakweli tuna kila sababu ya kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwenye maono na uongozi wake bora wa kujali, wananchi, maendeleo haya ambayo yamefanywa kwenye Halmashauri hii na Mkoa mzima wa Kilimanjaro ni makubwa na hayajawahi kutokea.” Alisema Waziri Mhagama.