SERIKALI imeanza kazi ya urejeshaji ya miundombinu ya kudumu ya barabara na madaraja katika sehemu zilizoathiriwa na mvua za Elnino na Kimbunga Hidaya mkoani Lindi.
Hiyo ni baada ya leo Oktoba 7, 2024 Wizara ya Ujenzi kutiliana saini na wakandarasi mikataba mitano ya ujenzi wa barabara na madaraja itakayosimamiwa na wakala wa barabara nchini Tanroads Mkoa wa Lindi chini ya ufadhili wa dharura wa miradi ya benki ya Dunia.
Tukio hilo lilishuhudiwa na Waziri wa Wizara hiyo, Innocent Bashungwa katika viwanja vya Shule ya Msingi Somanga, Wilayani Kilwa mkoani Lindi.
Barabara zilizotiliwa saini ambazo zilikatika ni barabara kuu ya Marendego -Nangurukuru -Lindi- Mingoyo katika maeneo ya Somanga Mtama, Songas, Mikereng’ende na Matandu.
Lakini pia, barabara ya Kiranjeranje -Namichiga hadi Ruangwa maeneo ya Kigombo na Nakiu, barabara ya Tingi -Chumo -Kipatimo katika maeneo ya Liomanga, Ngoge na Chumo pamoja na barabara ya Liwale -Nachingwea maeneo ya Nangano na Mbwemkuru II.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Bashungwa amesema Mkoa wa Lindi ndio uliopata bajeti kubwa kuliko mikoa mingine kutokana na mkoa huo miundombinu yake kuathiriwa zaidi.
Amesema Serikali imetenga kiasi cha Sh.Bilioni 140 katika miradi hiyo ya dharura na madaraja 13 yanakwenda kujengwa ili kurudisha mawasiliano kwa kujenga miundombinu ya kudumu itakayofanya wananchi wa kusini kufanya shughuli zao za kiuchumi na kusafiri kwa uhakika kutokana na kuwa na barabara zenye viwango.
Awali, akitoa taarifa ya miradi hiyo ya barabara Mtendaji Mkuu Tanroads, Mhandisi Mohamedi Besta amesema miradi hiyo itatekelezwa kwa kipindi cha miezi 10 ikigawanywa katika sehemu 13 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa daraja la mita 60 barabara unganishi eneo la Matandu -Njenga II, ujenzi wa makaravati saidizi na midomo mitano yenye ukubwa wa mapana ya mita tano katika daraja la Mbwemkuru.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amewataka wakandarasi waliopata zabuni ya kujenga kuhakikisha wanamaliza matengenezo hayo ndani ya miezi iliyopangwa, huku akiahidi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Mvua zilizoambatana na Kimbunga Hidaya zilizonyesha Februari hadi Mei, mwaka huu zilisababisha uharibifu mkubwa wa madaraja pamoja na barabara na hivyo kusababisha usumbufu wakati wa kusafiri.