Akizungumza leo Oktoba 7, 2024 jijini Dar es Salaam katika hafla fupi ya wiki ya huduma kwa Mteja, Mhandisi Mashola amesema kuwa kila mfanyakazi ana uwajibu wa kufanya kazi kwa ufanisi katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja.
Mhandisi Mashola amesisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora yenye viwango, huku akifafanua kuwa wameajiriwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi, kila mfanyakazi ana uwajibu wa kuwa na lugha rafiki wakati wa kutoa huduma kwa wateja.
“Katika majukumu yetu tunapaswa kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya wiki ya huduma kwa wateja ambayo kwa mwaka huu inasema : Kutoa huduma bora juu na zaidi ya matarajio ya Wateja kwa Shirika” amesema Mhandisi Mashola.
Amewakumbusha watanzania kuunga mkono juhudi za Rais Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani kwa kutumia nishati safi ya umeme kwa ajili ya kupikia kwa kutumia kutumia jiko janja.
Afisa Habari Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Temeke Lucia Renatus, amesema katika mkoa huo kuna wateja 249, 596 na kufanikiwa kupata mapato ya shilingi bilioni 20 kwa mwezi.
Amesema kuwa katika wiki ya huduma kwa mteja wamelenga kumsherekea mteja na mfanyakazi, huku akisisitiza kuwa kila mfanyakazi anapaswa kuongeza bidii katika utendaji kazi ili kuongeza mapato ya shirika.
“Lengo la kukutana hapa ni kujadiliana kwa pamoja namna gani tunaweza kufanya kazi zaidi ya matarajio kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wateja pamoja na kuongeza mapato ya shirika kwa kuuza umeme kwa wateja” amesema.
Amesema kuwa katika wiki ya huduma kwa wateja wanatarajia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ulinzi wa miundombbinu, mifumo inayotumika pamoja na matumizi ya nishati safi ya umeme.
Ameeleza pia watawatambua wateja ambao wamekuwa wakilipa huduma ya umeme kwa wakati bila ya usumbufu pamoja na viongozi kutengeneza miundombinu ya umeme.
Katika hafla fupi ya wiki ya huduma kwa wateja wafanyakazi bora TANESCO Mkoa wa Temeke wamepewa zawadi kwa ajili ya kutambua mchango wao pamoja wajadili mada mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kutoa huduma bora kwa wateja juu na zaidi ya matarajio kwa shirika.