MKURUGENZI Chama cha waandishi wa habari Wanawake (TAMWA ZNZ), Dk.Mzuri Issa amesema bado kuna changamoto zinazowakwamisha Wanawake kuwa viongozi ikiwemo unyanyasaji wa kundi hilo mtandaoni.
Akifungua mkutano wa wadau wa masuala ya wanawake na uongozi kupitia vyombo vya habari huko Ofisi za TAMWA Tunguu alisema hatua hiyo inachangia kuwavunja moyo na kuwarudisha nyuma Wanawake kugombea nafasi hizo.
“Bado kuna udhalilisha na irudishwaji nyuma wa Wanawake kugombea nafasi za uongozi ikiwemo kuogopa, kukatishwa tamaa, kukatazwa , na kukemewa kushiriki harakati za kisiasa” alisema Dk. Mzuri
Alisema lengo la chama hicho ni kuona haki za Wanawake wzinaimarishwa kwa njia mbali mbali ikiwemo kuwekewa mifumo ya kuwalinda kipindi cha siasa na itakayowawezesha kugombania nafasi za uongozi na kushinda.
Aidha alieleza kuwa chama hicho kinatamani kuona wanawake wananyanyuliwa na kuwekea mazingira mazuri ya kuwa salama mtandaoni wanaposhiriki katika nafasi za uongozi ili kufikia usawa wa 50 kwa 50.
“Watu wasiojiamini huandaa mikakati ya kuwarejesha nyuma wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi hivyo ni mwiko kuzungumzia masuala ya kurudi nyuma katika kufika usawa wa 50 kwa 50”. Alisema Dk. Mzuri
Afisa elimu kutoka Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi ZAECA Yussuf Juma Suleiman alisema wanawake wana nafasi sawa na wanaume kushiriki katika uongozi hivyo ni vyema kila mmoja kuchukuwa hatua kuhakikisha usawa katika nafasi za uongozi unapatikana.
Alifahamsha kuwa moja kati ya vikwanzo vinavyowarudisha nyuma wanawake katika kugombea nafasi za uongozi ni rushwa ya ngono ambapo sheria ya rushwa namba 5 ya mwaka 2023, kifungu cha 53 imeeleza mazingira ya ngono hivyo ni vyema wanawake kuyajua mazingira hayo ili kuwa mstari wa mbele kuzuia na kupambanana vitendo hivyo visitokee.
“Kabla wanawake hawajaingia katika kugombea nafasi za uongozi, ni vizuri kupewa elimu ya uraia, ili kujua miiko na misingi ya uongozi, ili wasiwe mwanya wa kutoa rushwa.” Alisema ofisa huyo
Ofisa sheria mwandamizi Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa Abdulrazak Said Ali, aliwataka wanawake kuwa na imani na ofisi hiyo kwani tayari imeanzisha dawati la jinsia kushuguhulikia masuala ya jinsia bila ya upendeleo wowote.
Wadau walioshiriki katika mkutano huo akiwemo Mwatima Issa Rashid na Nusra Shabani walisema uzowefu unaonesha kuwa changamoto ya uchumi bado inawarudisha nyuma wanawake kufikia malengo ya dhamira ya mwanamke kuwa kiongozi hivyo kuvitaka vyama vya siasa kuandaa Sera zitakazowewezezha Wanawake kiuchumi ikijumuisha kuweka mafungua maalum ya wanawake ili kuwasaidia kufikia malengo yao.
Aidha waliishauri ZAECA kutoa elimu ya kutambua mazingira ya rushwa ya ngono ila kujikinga na kuzuia kutokea kwa vitendo hivyo na kuwataka kuweka wazi Sheria za adhabu kwa wanaodhalilisha wanawake kupitia mitandao .
“Kuna haja ya kuwapatia Wanawake elimu ya uraia na stadi za maisha ili waweze kujitambua na kuepukana na kutumika vibaya na kuwa myanya ya rushwa ya ngono” walishauri wadau hao.
Hata hivyo waliishauri TCRA kuzuia taarifa zinazomvunjia uaminifu mwanamke kwa jamiii ili kuwa huru kutumia mitandao hiyo kwani mwanamke mtetezi lazima awe salama mtandaoni.
TAMWA ZNZ imeandaa kikao hicho kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa taasisi za Serikali na binafsi pamoja na waaandishi wa habari vijana ili kuwajengea uwezo wa kuandika na kuzifanyia uchambuzi habari zinazohusu wanawake na uongozi kupitia mradi wa wanawake na uongozi.