Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Bukene, wilayani Nzega Mkoani Tobora mara baada ya kukagua miradi
mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali mkoani humo Oktoba 8, 2024.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akisisitiza jambo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Bukene, wilayani Nzega mkoani Tabora wakati wa ziara ya Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango mkoani humo Oktoba 8, 2024
Wananchi wa Mkoa wa Tabora wakimsikiliza Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara mara baada ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali mkoani humo, Oktoba 8, 2024.
……….
Makamau wa Rais, Dkt, Philip Mpango amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika mkoa wa Tabora ili kuongeza
kasi ya uzalishaji wa mazao na kukuza uchumi wa Mkoa huo.
Akizungumza Oktoba 8, 2024 katika siku ya Kwanza ya ziara yake ya Siku Nne mkoani humo, Dkt. Mpango amewataka wananchi wa wilaya za
Igunga na Nzega kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa kuwa Serikali imedhamiria kujenga barabara za kisasa
zitakazorahisisha uchukuzi wa mazao hayo kutoka mashambani na kuyafikisha sokoni kwa urahisi.
“Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Kasekenya hakikisheni barabara zinapitika wakati wote na wakandarasi wanafanya kazi kwa wakati kwani fedha za ujenzi zipo”, amesema Dkt. Mpango.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya amesema Serikali imepanga kuijenga upya barabara ya Singida – Shelui- Nzega (Km 220).
Kasekenya ameongeza kuwa tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa sehemu ya Shelui –Nzega (Km 128) na Shelui – Singida (Km 92)
umekamiliika.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuongeza kasi ujenzi wa barabara ya Tabora- Mambali- Bukene- Itobo (Km 114) na sehemu ya Nzega – Itobo- Kagongwa (Km 65) ili kuunganisha mkoa wa Tabora na Shinyanga kwa njia fupi.
“Tumejipanga vizuri kuboresha miundombinu katika Mkoa huu, pamoja na ujenzi wa barabara hizi, pia zitawekwa taa katika maeneo ya miji na alama nyingine za barabarani ili kuzipendezesha na kuwawezesha wananchi kufanya biashara wakati wote”, amesema Kasekenya.
Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango anaendelea na ziara yake ya Siku Nne Mkoani Tabora ambapo kesho atakagua miradi ya maendeleo katika wilaya za Tabora na Uyui.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.