Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiweka Jiwe la Msingi Mradi wa Ujenzi wa Mabwawa ya Kutibu Majitaka uliopo katika eneo la Uchama Wilaya ya Nzega wakati akiwa ziarani mkoani Tabora tarehe 08 Oktoba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua Mradi wa Ujenzi wa Mabwawa ya Kutibu Majitaka uliopo eneo la Uchama Wilaya ya Nzega mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi katika mradi huo akiwa ziarani mkoani Tabora tarehe 08 Oktoba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria kukabidhi magari ya majitaka kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Nzega wakati wa hafla ya uwekaji Jiwe la Msingi Mradi wa Ujenzi wa Mabwawa ya Kutibu Majitaka uliopo katika eneo la Uchama Wilaya ya Nzega wakati akiwa ziarani mkoani Tabora tarehe 08 Oktoba 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Wananchi wa Nzega Mjini wakati akiwa ziarani mkoani Tabora tarehe 08 Oktoba 2024.
………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Maji kuendelea na kasi ya usambazaji maji kutoka Ziwa Victoria ili kutatua adha ya ukosefu maji waliyopata wananchi kwa muda mrefu.
Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Bukene unaogharimu shilingi bilioni 29.3 katika hafla iliyofanyika Kijiji cha Uduka Wilaya ya Nzega akiwa ziarani mkoani Tabora.
Ameipongeza Wizara ya Maji kwa kazi kubwa inayofanya kuhakikisha maeneo yaliokabiliwa na changamoto ya maji yanafikiwa hususani kwa kutumia chanzo cha ziwa Victoria.
Katika hafla hiyo Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa Tabora kuongeza juhudi katika kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ameitaka Wakala wa Misitu Nchini (TFS) kuhakikisha miche inapatikana ili kuwezesha wananchi kupanda miti wakati huu kipindi cha mvua kinapokaribia.
Amewahimiza viongozi kuongoza juhudi za upandaji miti na wananchi kupanda miti katika maeneo yao ikiwemo ya kivuli na matunda.
Aidha Makamu wa Rais amehimiza umuhimu wa kampeni ya kuwahamasisha wanafunzi wakati wakiwa masomoni kuwa na mti waliopanda na kuutunza ili wajifunze umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Vilevile Makamu wa Rais amesihi wananchi wa Bukene kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu.
Mradi wa Maji Bukene unatarajia kunufaisha wananchi 85,607 ukiwa na mtandao wa bomba za kilomita 193.5 ukitarajiwa kuwa na vituo vya kuchotea maji 91.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameweka Jiwe la Msingi Mradi wa Ujenzi wa Mabwawa ya Kutibu Majitaka uliopo eneo la Uchama Wilaya ya Nzega unaogharibu shilingi bilioni 1.5 unaotarajiwa kudumu kwa miaka zaidi ya 20.
Makamu wa Rais amesisitiza mradi huo kutumika katika kilimo cha umwagiliaji ili kuwa na manufaa zaidi na kuhakikisha maji hayo hayapotei bure.
Vilevile Makamu wa Rais amezungumza na wananchi wa Nzega Mjini katika eneo la Sokoni ambapo amesisitiza wafanyabiashara wadogo katika soko hilo watapewa kipaumbele cha kupata vizimba baada ya soko la kisasa kujengwa.